Mnyeti asitisha shughuli za kituo cha utafiti wa madini Hanang'

|
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesitisha shughuli za Kituo cha Utafiti wa Madini kiitwacho Kudu Resources kilichopo katika Kijiji cha Bassotu wilayani Hanang baada ya kubainika kinafanya shughuli za utafiti kinyume na taratibu.

Kituo hicho pia kimebainika kudaiwa kodi na serikali ambazo ni dola za kimarekani 68,000 na PIA kikidaiwa kupeleka sampuli za madini mkoani Mwanza bila kuwa na kibali.

Awali utafiti wa kituo hicho ulieleza kuwa wamegundua kuna viashiria vya madini ya dhahabu katika kijiji hicho cha Bassotu kilichopo wilayani Hanang mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti kituo hicho kimekuwa kikifanya shughuli kinyume na taratibu na kwamba tangu waanze kufanya utafiti mwaka 2011 hadi leo serikali haijanufaika na utafiti huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo hicho, Wiliam Lazaro amekiri kudaiwa kodi na serikali sanjari na kudai kuwa kwa sasa hawafanyi chochote zaidi ya kuweka kambi tu, wakati wakisubiri leseni na vibali vinavyohusika.

Imeelezwa kuwa utafiti wa madini ya dhahabu katika Kijiji cha Bassotu ulianza tangu mwaka 2011 na kwamba hadi leo bado hawajatoa taarifa za utafiti huo.

Madini
Maoni