Mnyeti awatisha TARURA, aahidi kumwandikia JPM barua

|
Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa, ikijadili kukwama kwa ujenzi wa miundombinu mkoani Manyara

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewaonya Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA) juu ya utekelezaji wa ahadi za Rais baada ya wakala hao kushindwa kuanza utekelezaji wa ahadi zake za ujenzi wa barabara katika maneo mbalimbali mkoani humo.

Mnyeti ametoa kauli hiyo katika kikao chake cha Kamati ya Ushauri ya mkoa ambapo amesema kuwa atamuandikia Rais barua ya kumueleza namna ambavyo TARURA wanavyochelewesha utekelezaji wa ahadi alizozitoa 2017 wakati akiwa katika ziara mkoani Manyara.

“Huu ni utetezi tu, kwanini tusimuandikie Rais kwamba ile ahadi uliyotoa TARURA wanakataa kutekeleza kutokana na kisingizo cha bajeti. Rais ana ahadi nyingi ninyi mlitakiwa kumkumbusha kwani nyingine hakumbuki. Kama mnaniruhusu niipeleke barua hiyo leo” alisema Mnyeti.

Pamoja na mambo mengine wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa wameiomba serikali kuiongezea bajeti ya fedha TARURA ili kuwasaidia kutekeleza uimarishwaji wa miundombinu ya barabara zilizo chini yao.

Wajumbe hao wamesema, TARURA amekuwa na kazi nyingi lakini kinachokwamisha utekelezaji huo kwa wakati ni uhaba wa bajeti na kuishauri serikali kutoa fedha ya kutosha kwa wakala hao waliopewa jukumu kubwa.

Hata hivyo Wakala huyo wa Barabara Mjini na Vijijini wakijitetea kuhusu malalamiko hayo wamekiri uwepo wa ufinyu wa bajeti unaopelekea kushindwa kuboresha miundombinu kwa wakati.

Miundombinu
Maoni