Mradi wa ofisi za wizara Ihumwa zawanufaisha wengi Dodoma

|
Waziri mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika ukaguzi wa ofisi za serikali za Ihumwa
Serikali imeeleza kuwa takribani shilingi bilioni 50 zimewanufaisha wakandarasi na wananchi wa hali ya chini wakati wa ujenzi wa ofisi za wizara mbalimbali katika Mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma.
 
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea takribani 13 zilizojengwa katika Mji huo wa Serikali uliopo eneo la Ihumwa.
 
Dkt. Mpango amesema kuwa katika eneo la ujenzi kulikuwa na mafundi kutoka kila pembe ya nchi, wafanyabiashara wadogo wa chakula (mama lishe) na wakandarasi ambao wamenufaika na uwekezaji mkubwa wa majengo ya ofisi hizo za Serikali katika eneo hilo la Ihumwa.
 
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa majengo hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepongeza maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hizo ambao umekamilika kwa asilimia 99 na kuagiza kasoro alizobaini zifanyiwe marekebisho pamoja na kuboreshwa kwa mazingira akiagiza kuwepo kwa bustani nzuri katika eneo hilo, kusawazisha eneo hilo na kuweka samani katika ofisi hizo ili ziweze kutumika.

Aidha, amemtaka mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kurekebisha kasoro alizozibaini hususan mlango mkuu wa kuingia ofisi hizo kabla ya kuzinduliwa rasmi na Rais hivi Karibuni.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Khatib Kazungu amesema Wizara imepokea maelekezo ya Waziri Mkuu na kuahidi kuyatekeleza kwa haraka ili watumishi waanze kutumia ofisi hizo.

Mhandisi kutoka NHC, anayesimamia ujenzi huo Elisante Ulomi ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano waliompa katika kufanikisha ujenzi huo ulioanza Disemba 29, 2018 na kuahidi kurekebisha kasoro zilizobainishwa wakati wa ukaguzi huo.

Biashara
Maoni