Mrema agoma kuwaunga wapinzani wenzake mkono

|
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema,

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, amesema hawezi kuungana na vyama vingine vya upinzani vilivyofungua kesi kupinga Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwake Salasala, Dar es Salaam, Mrema amesema wapinzani wanapaswa kufahamu kuwa hitaji la sasa la nchi ni marekebisho ya sheria kwa ujumla na si sheria moja moja.

Amesema anaamini kufanya hivyo hakuwezi kuondoa matatizo yaliyopo ambayo msingi wake unatokana na ubovu wa sheria zilizopo.

“Siwezi kuungana na wapinzani kumshtaki AG, hii nchi inahitaji marekebisho makubwa ya sheria zinazotumika. Kwa uzoefu wangu wa kisiasa na nyadhifa nilizowahi kushika ikiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, kuna haja ya kufanya marekebisho, hii itasaidia pia kuwalinda viongozi akiwamo Rais,” alisema Mrema.

Alisema anaamini mawazo ya wapinzani wenzake kuupinga muswada huo ni mazuri, lakini jambo hilo litafanikiwa na kuwa na tija kama wanalifanya kwa nia nzuri kwa taifa.

Mrema ametoa kauli hiyo ikiwa ni kadhaa zipite baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuanza kusikiliza kesi namba 31 ya kupinga muswada huo iliyofunguliwa mahakamani hapo Desemba 20, mwaka jana na viongozi wa vyama vya upinzani.

Viongozi waliofungua kesi hiyo ni pamoja na  Kiongozi Mkuu ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Kaimu Katibu Mkuu CUF (Bara), Joram Bashange na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani.

Katika kesi hiyo mshtakiwa mkuu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilangi.

Siasa
Maoni