Msaada wa haraka wa uokozi wahitajika kwa waliokwama Msumbiji

|
Msumbiji: Watu wanaodhaniwa wa familia moja wakiwa wamezungukwa na maji kwenye moja ya maeneo ya mji wa Beira ulioathiriwa vibaya na kimbunga Idai.

Mamlaka nchini Msumbiji zimesema kuwa takribani watu 15,000 wanahitaji msaada wa haraka wa kuokolewa baada ya kukwama kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo walipokuwa wakijihifadhi kufuatia athari za kimbunga Idai.

Takribani watu 300 wamethibitika kufariki dunia nchini Msumbiji na Zimbabwe lakini idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Kwenye mji wa bandari wa Beira, watoaji misaada wamesema wamebakiwa na maji safi ya kunywa yanayoweza kutosheleza kwa siku mbili au tatu tu.

Kimbuka kikali cha Idai kilichokuwa kikisafiri kwa kasi ya zaidi ya kilomita 177 kwa saa, sawa na mita 106 kwa saa kiliukumba mji wa Beira Alhamisi iliyopita na kuharibu makazi ya watu sambamba na kusukumia maji kwenye makazi hayo na kufanya sehemu kubwa ya mji huo kufunikwa na maji.

Mashirika ya afya yameonya kuwa ukosefu wa chakula na maji safi unaweza kupelekea hatari mpya ya mlipuko wa magonjwa.

Maisha
Maoni