Muheza washauriwa kusafisha mashamba yao kudhibiti panya

|
Moja ya shamba lililoathiriwa na baa la panya

Wakulima  wilayani  Muheza ,wametakiwa kuwa na utaratibu wa kusafisha mashamba yao mara baada ya mavuno  ili kuepuka wadudu waharibifu kama  Panya ambao wanaingia shambani na kushambulia mazao yao.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Uthibiti Baa la Panya  kutoka Morogoro,  Emanuela  Celestina wakati akizungumza na wakulima wa  Kata ya Mhamba  na Songa zilipo wilayani humo.

Kwa takriban miaka miwili mfululizo wakulima wengi wilayani Muheza wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la panya kuvamia mashamba yao na kuharibu mazao  lakini kwa kipindi hiki tatizo hilo limedaiwa kuongezeka mara dufu.

Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wakulima waliokumbwa na kadhia hiyo wamesema kutokana na panya hao mazao waliyolima mwaka huu yameharibiwa kabisa yakiwemo mahindi, mihogo na mpunga.

Diwani wa Kata ya Mhamba, Geofrey  George amesema kwa kata yake pekee yenye kaya  891 jumla ya hekta 171 zimeharibiwa.

Kufuatia tatizo hilo  mtaalam wa Kilimo kutoka Kituo cha Udhibiti Baa la Panya, Morogoro akifuatana na Afisa Kilimo wa Wilaya ya Muheza wamefika katika vijiji vinne vya Kata ya Mhamba na Songwe na kugawa sumu ya Panya  kwa wakulima hao na kuwataka kusafisha mashamba yao mara kwa mara huku wakiwasisitiza kutembelea mashamba kila mara.

Wataalamu hao wamesema kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa nchini, wakulima wote wanapaswa kuyalinda mashamba yao kwa kusafirisha ili kuwadhibiti panya hao kutokana na serikali kutokuwa na uwezo wa kununua sumu hiyo nchi nzima kwa sababu za gharama yake kuwa kubwa.

Kilimo
Maoni