Nditiye awahakikishia Lindi na Pwani mawasiliano ya uhakika

|
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza na wananchi wa vijiji vya mkoa ya kusini

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amewahakikishia wananchi wa baadhi ya vijiji ambavyo havina mawasiliano mkoani Lindi na Pwani kuwa Serikali inahakikisha kuwa wananchi waishio kwenye vijiji hivyo wanapata huduma za mawasiliano ya uhakika

Nditiye ameyasema hayo akiwa kwenye ziara yake ya kukagua changamoto za hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio maeneo ya Liwale, Lindi Vijijini, Mtama, Kibiti na Rufiji kwenye Mkoa wa Lindi na Pwani baada ya kupata kilio kutoka kwa wabunge wanaowakilisha wanananchi wa maeneo hayo wakati wa Kikao cha Bunge mwezi Novemba mwaka huu.

Amesema Sekta ya Mawasiliano ni sekta inayoshika nafasi ya pili kwa kuchangia Pato la Taifa katika kipindi cha mwaka 2016/2107 kwa kiwango cha asilimia 13.1 ambapo mawasiliano pekee yanachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa.

 “Wananchi mkiwasiliana kwa kununua vocha, kupiga simu na kutumia intaneti, Serikali inatoza kodi kidogo, ambayo wala haiumizi na wala mwananchi hausikii, lakini Serikali inapata mapato yake,” alisema Nditiye.

Amefafanua kuwa ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma za mawasiliano na kwamba hadi sasa asilimia 94 ya wananchi wote wanawasiliana kwa kuwa Serikali imeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao unatoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi ili ziweze kupeleka huduma za mawasiliano kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara

Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Sara Chiwamba amemshukuru Nditiye kwa ziara yake Liwale na kufika Mirui kuzungumza na wananchi ambao wana kiu ya kupata mawasiliano.

“Tuna imani mawasiliano yatapatikana kwa kuwa mawasiliano yanasaidia ulinzi na usalama na Wilaya yetu itaenda kufunguka,” alisema Chiwamba.

Naye Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka amemweleza Nditiye kuwa mradi huu wa mawasiliano kwenye Kata ya Mirui ni miongoni mwa miradi sita inayotekelezwa na UCSAF na ni matumaini kuwa hadi Januari 2019, Mirui watakuwa wameunganishwa na dunia kupitia mawasiliano.

Naye Mkuu wa Wilaya la Lindi, Shaibu Ndemanga amemshukuru Nditiye kwa kufika na kufanya mkutano na wananchi wa Kijiji cha Chihuta kilichopo Mtama, Lindi kwa kuwa wamekosa mawasiliano kwa muda mrefu Ilhali wana uchumi mzuri wa korosho.

Nditiye amesema kuwa, “nitafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Chihuta mnapata mawasiliano kwa kuwa mawasiliano ni uchumi na ni maendeleo,”.

Nditiye ameilekeza UCSAF ifike Chihuta ndani ya mwezi mmoja ifanye utafiti na kujenga mnara wa mawasiliano. Pia ameongeza kuwa kwenye Jimbo la Mtama ipo miradi nane ya mawasiliano na miradi mingine sita inaongezwa na mwezi Machi mwakani na zabuni nyingine itatangazwa na UCSAF ili kampuni za simu ziweze kuomba kwa lengo la kujenga minara ya kufikisha huduma za mawasiliano ili wananchi wawasiliane.

Biashara
Maoni