Peter Tino akabidhiwa zawadi ya milioni 5 alizoahidiwa na Rais Magufuli

|
Peter Tino amekuwa sehemu ya wachezaji wa zamani wa Taifa Stars walioshiriki kwenye kamati ya kuhamasisha wachezaji wa Taifa Stars kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Uganda.

Mfungaji wa bao lililoiwezesha Taifa Stars kutinga kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya Afrika mwaka 1980, Peter Tino amekabidhiwa pesa taslim Shilingi milioni 5 alizopewa na Rais John Magufuli.

Mchezaji huyo wa zamani wa Stars amekabidhiwa fedha hizo leo kufuatia kauli ya Rais aliyoitoa mapema ikulu jijini Dar es Salaam wakati alipowaalika wachezaji wa Taifa Stars, Kamati ya kuhamasisha ushindi dhidi ya Uganda na bondia Hassan Mwakinyo ili kuwapa pongezi kwa ushindi walioupata.

Taifa Stars iliweka historia ya kurejea kwenye michuano mikubwa zaidi barani Afrika baada ya miaka 39 kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya majirani zao wa Uganda kwenye mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa.

Mshambuliaji wa Stars anayekipiga nchini kwenye klabu ya Difaa El Jadid ya nchini Morocco alifungua ukurasa wa mabao kwa kumalizia pasi safi ya John Bocco kwenye dakika ya 21.

Walinzi wawili wa Taifa Stars walifunga mabao mawili ya haraka haraka ndani ya muda wa dakika saba wakati mlinzi wa Simba SC, Erasto Nyoni akifunga mkwaju wa penati kwenye dakika ya 51 huku mlinzi wa Azam FC, Agrey Morris alipomalizia kwa kichwa krosi ya John Bocco na kukamilisha ushindi wa kihistoria kwa Stars ambao uliwapa tiketi ya fainali ya AFCON zitakazopigwa nchini Misri.

Rais Magufuli ametoa zawadi ya kiwanja cha makazi kwa kila mchezaji wa Taifa Stars mkoani Dodoma sambamba na fedha taslimu shilingi milioni 10 ambapo Peter Tino nae amejumuishwa kwenye zawadi ya kiwanja.

Fainali za AFCON zitafanyika mwezi Juni nchini Misri huku makundi yakitarajiwa kupangwa baadae wiki hii.

Soka Tanzania
Maoni