Picha za vijana wa Thai baada ya kuokolewa zatolewa rasmi

|
Baadhi ya vijana waliokolewa kwenye pango waonekana wakiwa hospitali wakiwa wanaendelea vyema

Picha za mwanzo zimetoka zikiwaonesha vijana 12 waliokuwa wamekwama kwenye Pango lililokuwa limezingirwa na mafuriko pamoja na kocha wao wakiwa katika wodi maalum katika Hospitali moja mjini Chiang Rai nchini Thailand.

Katika picha iliyopigwa kwa mbali, imewaonesha vijana hao wakiwa wamevaa vifaa vya hewa puani na magauni ya hospitali na kuonesha ishara ya ushindi mbele ya kamera.

Picha hiyo imepigwa na kutolewa kama taarifa mpya kufuatia jitihada kubwa iliyofanyika wakati wa kuwatoa nje watoto hao waliokuwa katika mazingira makubwa.

Kikosi cha wanamaji wa Thai nao wametoa video yao inayoonesha namna zoezi hilo lilivyoendeshwa kwa mafanikio.

Watoto hao wanadaiwa kupungua sana uzito kutokana na mazingira waliyokuwa nayo, na kwa mujibu wa wizara ya afya, kundi la kwanza la vijana wanne, tayari wamefanikiwa kuonana na familia yao na kuanza kula chakula cha kawaida huku kundi la pili likitarajiwa kuonana na familia zao kesho na leo, Jumatano walitarajiwa kuanza kula chakula cha kawaida.

Kwa sasa vijana hao wote 13 wanaendelea na matibabu katika hospitali ya mji wa Chiang Rai  pamoja na kupatiwa msaada wa kisaikolojia, huku ikidaiwa kuwa  wanaendelea vizuri.

Maisha
Maoni