Polisi Mwanza wafanikiwa kuwatia mbaroni majambazi sugu

|
Kamanda Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na kikosi kazi cha kanda ya ziwa kimefanikiwa kuwakamata jumla ya majambazi watano sugu wakiwa na noti bandia zenye thamani ya kiasi cha milioni 2.8 na vifaa mbalimbali vya kutengenezea fedha hizo huko mtaa wa Kiloleli B, Kata ya Nyasaka wilayani Ilemela, kitendo ambacho ni kosa la jinai.

Katika operesheni hiyo maalumu iliyochukua takbrani saa 48 imefanyika baada ya kupatikana kwa  taarifa za kiintelejensia kwamba katika mtaa huo wa Kiloleli B wapo watu wanaotengeneza noti bandia.

Kwa mujibu wa Kamanda Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana amesema ukamataji huo umefanikiwa kutokana na ushirikiano wa kikosi maalumu cha askari wa mikoa ya kanda ya ziwa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Tanapa.

Amesema kati ya watuhumiwa hao wawili wamekamatwa katika maeneo ya Mugumu Serengeti ambao ni Swedi Amani Mrete aka Kongo mwenye miaka 40, mfanyabiashara na mkazi wa Buhongwa Mwanza,  Cosmas Busiga Bereka mwenye miaka 40 ambaye ni fundi chuma na Mkazi wa Mandu Mwanza.

Aidha watuhumiwa wengine wawili walikamatwa katika Mtaa wa Kiloleli B kwenye nyumba ambayo ndipo walipokuwa wakitengenezea fedha hizo bandia ambao ni Baraka Dominiko mfanyabiashara na mkazi wa Kiloleli B, Khadija Musa Elias mwenye miaka 20, mkulima na Mkazi wa Kiloleli B huku mwingine akikamatwa baadaye baada ya kufanikiwa kutoroka.

Uhalifu
Maoni