Polisi watakiwa kumaliza upelelezi wa kesi za ubakaji haraka

|
Vijana wakiwa katika maandamano ya Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia kwa wanawake na watoto

Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imetakiwa kuhakikisha kuwa hadi mwisho wa mwaka huu upelelezi wa zaidi ya matukio 500 ya ubakaji uwe umekamilika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria lengo likiwa ni kuyadhibiti matukio hayo katika jamii.

Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alipokuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo takwimu zilizotolewa na Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam zinaonesha kuwa kwa mwaka huu matukio 714 ya ubakaji yameripotiwa.

Kati ya matukio hayo, 539 yapo katika ngazi ya upelelezi huku 175 kesi zake zipo mahakamani ambapo watuhumiwa 158 wanashikiliwa na Polisi.

Akizungumzia takwimu hizo, Mkuu huyo wa wilaya amesema, ni wakati sasa wa kufikishwa mahakamani wahalifu hao ili ije kuwa funzo kwa wanaume wanaoharibu mabinti.

“Ni lazima watu hawa wachukuliwe hatua haiwezekani mwanaume wa miaka 50 unamuingilia mtoto wa miaka minne , wewe ni lazima utakuwa huna akili na lazima wafungwe” alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ameahidi kulishughulikia suala hilo na kuwaonya wote wanaojihusisha na vitendo hiyo kuacha mara moja.

Kwa upande wa wananchi waliozungumzia matukio hayo wamesema, wazazi wanapaswa kuwalinda watoto wao sambamba na kukomeshwa kwa tabia ya baadhi ya wazazi kuwafichia siri watoto wao na wale waliowatendea ukatili huo huku kesi nyingine zikimalizwa kwa siri.

Uhalifu
Maoni