Polisi watoa neno kuhusu kupigwa kwa mwandishi Mbise

|
Kamanda Kanda maalum, Lazaro Mambosasa
Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, limesema tayari limeshafungua jalada la uchunguzi kuhusu tukio la kupigwa kwa mwandishi wa habari, Sillas Mbise lililotokea Agosti 8, wakati wa mchezo kati ya Timu ya Simba na Asante Kotoko jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza na waandishi wa Habari, Kamanda wa Kanda maalum, SACP Mambosasa amesema, hawatafumbia macho ukiukwaji wa sheria iwapo utafanywa na askari na kwamba iwapo itabainika kutenda kosa hilo hatua kali kwa mujibu wa sheria zitachukuliwa.
 
Mambosasa amesema, imeanza uchunguzi kupitia video ya kushambuliwa kwa mwandishi huyo inayosambaa mitandaoni na kumtaka mwandishi huyo kwenda kituo cha polisi kutoa taarifa juu ya shambulio hilo.
 
Mambosasa amesema, kazi ya Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao na kusema hairuhusiwi polisi kushambulia raia aliyetii sheria.
 
Sillas Mbise inadaiwa alishambuliwa na Polisi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Simba na Asante Kotoko katika kuadhimisha ya Simba.
 
Wakati huo Chama cha waandishi wa habari za michezo (TASWA) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) wametoa matamko ya kulaani kitendo hicho kilichotokea Jumapili.
Utawala
Maoni