Test
Waliokufa katika kampeni Nigeria wafikia 15

Idadi ya watu waliofariki dunia kwenye Kampeni za Mgombea wa Chama Tawala Nchini Nigeria, Muhammadu Buhari imeongezeka na kufikia watu 15 kutoka watu saba waliokufa siku ya kwanza kwa mkanyagano.

Duru za kitabibu zimebainisha idadi hiyo imeongezeka baada ya eneo hilo kufanyiwa usafi na kukutwa miili ya watu wengine saba waliohudhuria kwenye kampeni hizo za uchaguzi zilizofanyika siku ya Jumamosi.

Msemaji wa Hospitali ya Chuo Kikuu Cha Port Harcourt, Kem Daniel Elebiga amesema wamepokea jumla ya miili ya watu hao 15 waliokufa kwenye kampeni hiyo.

Amesema miili iliyopokewa ni ya wanaume watatu na wengine saba ni wanawake ambapo jumla ya watu waliojeruhiwa ni 12 na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Kampeni za lala salama zimeendelea kuwa kali ambapo upande wa Rais Buhari anaendelea kupambana kuhakikisha anarejesha tena kiti chake anachokishikilia.

Mwenyekiti wa Baraza la madiwani Babati ang'olewa

Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Babati Mkoa wa Manyara limemuondoa katika nafasi ya uenyekiti aliyekuwa mwenyekiti Mohamed Kibiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutokana na kukabiliwa na shutuma za kujihusisha na matumizi mabaya ya madaraka akituhumiwa kuwa na maslahi binafsi na Kampuni YA HAPPY MARK.

Inadaiwa kuwa Kampuni hiyo imepewa zabuni ya ukusanyaji wa mapato katika vyanzo zaidi ya vitatu vya halmashauri hiyo huku ikidaiwa kushindwa kupeleka asilimia 40 ya mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo ya jamii.

Diwani huyu aliipata nafasi  hiyo ya uenyekiti baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 akitokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kupata kura nane kati ya 12 kwa kuwa kipindi hicho madiwani wa chama chake walikuwa ni wengi kuliko wa Chama Cha Mapinduzi.

Safari ya kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Halamashauri ya Mji wa Babati inahitimishwa kwa kupigwa kura za ndiyo na hapana ambapo kura nne pekee ndizo zilimtaka abaki katika nafasi hiyo na kura nane zikimtaka aondoke.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Fortunatus Fwema baada ya matokea hayo akatolea ufafanuzi hatua zaidi zilizomuondoa kiongozi huyo kwenye nafasi hiyo ya uenyekiti ambazo alizitaja kuwa ni maslahi binafsi katika utoaji zabuni, ameshindwa kubuni vyanzo vya mapato pamoja na kashfa zinazomkabili huku Mbunge Jimbo la Babati, Paulina Gekul akisema hatua hiyo ni ushindi kwao kutokana na kwamba haki imetendeka kwa kumuondoa kwa njia ya demokrasia kutokana na kutokuwa na Imani naye kabisa.

Kwa upande wake, aliyekuwa mwenyekiti huyo amesema, kilichofanyika siyo haki kwa madai kuwa kushindwa kwake kuongeza mapato kulitokana na vyanzo vingi kuchukuliwa na serikali kuwa na wao kuwa katika mkakati wa kujipanga kuvumbua vipya.

Kufuatia madiwani watatu pamoja na mbunge kuhamia CCM wakitokea Chadema kunaifanya Halmashauri ya Mji Babati kuwa na madiwani  Wanane (8) huku CHADEMA ikisalia na Wanne (4).

Mkapa aamua kupumzika kutatua mgogoro wa Burundi

Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameachia ngazi nafasi ya kuendelea kuwa msuluhishi katika mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini Burundi, msemaji wake ameieleza BBC.

Mgogoro huo wa kisiasa ulipamba moto mwaka 2015 baada ya Rais wa sasa Pierre Nkurunziza kujiongeza muhula wa tatu ulioleta sintofahamu nchini humo na kupingwa vikali na upinzani.

"Kipindi cha kusuluhisha kimefikia mwisho,’’alinukuliwa akisema Makocha Tembele.

Hata hivyo msemaji huyo amekanusha kuwepo kwa taarifa zinazodai kuwa Rais Mkapa amejiuzulu nafasi hiyo.

"Ni mwisho wa mamlaka yake," alisema, na kuongeza kuwa Mkapa ameshawasilisha ripoti yake ya mwisho wakati wa mkutano wa mwisho wa viongozi wakuu wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika mapema mwezi huu.

Tembele amesema kilichobaki ni kwa upande wake Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuendelea na awamu inayofuata ya usuluhishi ambayo inapaswa kufanyika kabla ya uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Hata hivyo mazungumzo hayo yalitokana na vurugu zilizotokea nchini humo na kuuawa watu takribani 1,000 yanaonekana kutofanikiwa kutokana na Serikali kwa mara kadhaa kugomea kutuma ujumbe katika vikao vinavyoitishwa na wasuluhishi hao.

Serikali ya DR Congo yatetea ulipaji wa marupurupu ya mawaziri

Serikali ya Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo (DRC) imetetea maagizo yanayoruhusu mawaziri kulipwa mishahara na marupurupu kwa maisha yao yote huku idadi kubwa ya raia wake nchini humo wakiishi katika umaskini.

Katika taarifa iliyotolewa mapema jana, Serikali imesema malipo hayo ya dola 2000 kwa kiwango cha chini si ya kuwatajirisha maafisa hao kama inavyoelezwa na wakosoaji.

Taarifa hiyo imesema Serikali inayoondoka nchini DRC ilikuwa inawapatia mawaziri "kiwango cha chini kuwatosheleza mahitaji yao ya kimsingi, kama chakula, makazi na huduma ya afya".

Waziri Kalemani awashukia wakandarasi wanaokataa kupokea maombi ya REA kwa ukosefu wa nguzo na nyaya

Waziri wa Nishati Medard Kalemani ameagiza wakandarasi nchi nzima pamoja na mameneja wa mikoa yote kupokea maombi ya wananchi ya kuunganishiwa umeme katika mradi wa REA badala ya kukataa kupokea maombi hayo kwa visingizio ya kutokuwa na miundombinu ikiwemo nguzo, na nyaya za umeme.

Waziri Kalemani ametoa maagizo hayo mkoani Geita alipokuwa akizingumza na wananchi wa kitongoji cha Ipandanshimba wilayani Chato.

“Pokeeni maombi yao na pindi mnapopata miundombinu ikiwemo nguzo na nyaya inakuwa rahisi kuwafungia badala ya kuanza tena kuwatafuta” Amesema waziri Kalemani

“Iwapo itabainika kiongozi yeyote anakataa kupokea maombi ya wananchi wanaotaka kuunganishiwwa umeme wa REA, hatua zitachukuliwa dhidi yake kwa kukwamisha jitihada za Serikali” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, waziri Kalemani amewataka wakandarasi wanaoshughulika na mradi wa REA kuwasha umeme kwenye nyumba zote bila kujali aina za nyumba hizo.

“Nawataka wakandarasi wawashe umeme kwenye nyumba za tembe, majani, makuti na hata ikiwezekana kama ipo kwenye mti. Lengo la Serikali ni kuwawashia wnanchi wake umeme hususani wale waishio vijijini”.

Rais Paul Kagame apokea kijiti cha Museveni

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenye mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi za EAC unaofanyika jijini Arusha akichukua nafasi ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Mkutano huo umehudhuriwa na marais kutoka, Tanzania, John Magufuli, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Makamu wa kwanza wa Rais wa Burundi na Mwakilishi kutoka Sudan Kusini.

Wakati huo huo, Jaji Sauda Mjasiri kutoka Tanzania amekula kiapo cha kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki katika mkutano uliofanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi na wanafunzi walioshiriki shindano la insha la Afrika Mashariki ambapo washindi mbalimbali walikabidhiwa zawadi.

Akizungumza kwa kifupi mara baada ya kukabidhi nafasi hiyo, Kagame ameahidi kutumikia nafasi hiyo kwa kadri ya uwezo wake, na kushirikiana na wenzake kwa maendeleo ya ukanda wote wa Afrika Mashariki.

Mkutano huo wa 20 wa kawaida wa Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha Februari mosi ambapo masuala mbalimbali yamepitishwa kwa maendeleo ya Afrika Mashariki inayokadiriwa kuwa na watu takribani milioni 150.  

Marais EAC wakutana Arusha

Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wapo Arusha katika mkutano wa 22 wa wakuu wa nchi.

Mkutano huu awali ulikuwa ufanyike mwishoni mwa mwaka jana lakini uliahirishwa kutokana na kutotRamia kwa akidi. Pia ulipopangwa ukaahirishwa tena.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ya sasa ilizinduliwa upya Novemba mwaka 1999 baada ya ile ya awali kudumu kwa miaka 10 tu kati ya 1967 na 1977 na kuvunjika kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na itikadi za kisiasa.

Wanachama wa EAC ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.