Pwani wafanikisha mpango wa anuani za makazi

|
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ikikagua utekelezaji wa mradi wa anuani na postikodi unaotekelezwa mkoani Pwani

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi na postikodi Kibaha mkoani Pwani na kubaini kuwa utekelezaji wa mpango huo utafungua uchumi wa viwanda mkoani humo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Selemani Kakoso wakati wa kikao cha pamoja baina yake na wajumbe wa Kamati hiyo baada ya kuhitimisha ziara yao ya kukagua utekelezaji wa mpango huo.

Kamati hiyo Iliongozwa na uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakiongozwa na  Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Jim Yonazi na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Asumpta Mshama na watendaji wengine kutoka wizarani na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kakoso amesema kuwa anuani za makazi na postikodi ni muhimu kwa kuzingatia kuwa mkoa wa Pwani ni mkoa ambao una uwekezaji mkubwa wa sekta ya viwanda kwa hiyo ni vema kukawa na anuani za makazi kama tulivyoshuhudia

Kakoso amesema kuwa wameiomba Serikali iwekeze fedha za kutosha kwa ajili ya mradi kama huu kwa kuwa utasaidia kutoa utambuzi kwenye maeneo mbali mbali hata wale wageni watakaokuja kuwekeza huku watakuta miundombinu imeshaandaliwa ambayo itasaidia kufahamu kwamba eneo hili limewekwa miundombinu ya Sekta ya Mawasiliano

Pia, ameishauri Serikali waendelee kulinda miundombinu inayowekezwa kwa kuwa watanzania walio wengi wana asili ya uharibifu hususan kwenye miundombinu na wanachukulia kama chuma chakavu, uwekezaji uweze kulindwa na Serikali ielimishe wananchi wafahamu na kutambua kuwa mradi huu ni wa kwao

Kakoso amefafanua kuwa kazi ya Bunge ni kuangalia fedha zilizowekezwa ambazo zimepitishwa na Bunge na tunapokuja kwenye ziara tunaangalia na kuhakikisha fedha zimefanya kazi ipi na halmashauri ipi imenufaika ili tuweze kupitisha fedha nyingine wakati wa bajeti ya Serikali

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa ameishukuru Kamati kwa kutembelea mradi wa anuani za makazi na postikodi ambapo hadi sasa utekelezaji umefanyika kwenye halmashauri 12 na baadae utekelezaji utafikia halmashauri 18.

“Mradi huu una faida nyingi ambazo zimesemwa ambapo tunahitaji kuhama tupate huduma za kimtandao ambapo tunapodumbukia kwenye uchumi wa kati na nchi ya viwanda, wazalishaji wetu waweze kuuza kupitia njia ya mtandao, kama tunavyoona hata sasa hivi vijana wengi wanafanya biashara kupitia njia ya mtandao, tunataka tuone kama Wizara tunatoa mchango mkubwa kwa kuboresha anuani za makazi na postikodi kufanya shughuli mbali mbali ziweze kwenda,” amesema Kwandikwa.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa utekelezaji unaendelea ambapo mkandarasi ambaye ni Chuo cha VETA, Dodoma kinafanya kazi ya kujenga miundombinu ya anuani za makazi na postikodi na itasaidia kufungua Tanzania ili iweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidunia kama ambavyo watu wanaweza kununua vitu kutoka nchi za mbali, tunataka watu waweze kununua huduma na bidhaa kutoka nchini kwetu.

“Mpango wa anuani za makazi na postikodi utasaidia sana utambuzi wa mahali bidhaa na huduma zilipo, uzalishaji na viwanda vilipo hata kama mtu anatoka China, Urusi, Ujerumani anaweza kujua kabisa kitu anachotafuta kiko wapi na mahali halisi ambapo tayari pameshapewa anuani za makazi. Tunaamini baada ya muda si mrefu, nchi yetu nayo itakuwa ni moja ya nchi ambazo itakuwa inaongoza kwa utambuzi wa mahali, makazi ya watu, maeneo ya viwanda na maeneo mbali mbali ili biashara iweze kukua na kuleta tija kwa uchumi wetu,” amesisitiza Dkt. Yonazi

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Pwani ambapo utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi na postikodi unaendelea, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Asumpta Mshama amesema kuwa uwepo wa mpango huo utawasaidia kujua mtu gani yuko wapi, kitu gani kiko wapi kwa kuwa mkoa wa Pwani ni ukanda wa viwanda na kwa kitendo hiki tumeingiza Tanzania katika ulimwengu hivyo itarahisha mambo mbali mbali ya kibiashara na itakuza uchumi wetu

Naye Mkuu wa Chuo cha VETA, Dodoma, Ramadhani Mataka, ameishukuru Wizara kwa kuipa VETA kazi ya kuwa mkandarasi wa utekelezaji wa mpango huo  ambapo kazi wanayoifanya imewanufaisha wanafunzi kwa kuwa uchumi wa viwanda hauwezi kusimama bila VETA. Pia, ameongeza kuwa VETA wametoa ajira kwa mafundi waliopo kwenye jamii na wamechangia mapato ya Serikali kwa kulipa kodi ya Serikali kiasi cha shilingi milioni 218

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema kuwa hadi sasa  utekelezaji umefanyika kwenye kata 112 nchini kwenye maeneo mbalimbali na kwameshatumia shilingi bilioni mbili kutekeleza mpango huo na kazi hiyo inaendelea. Mhandisi Ichwekeleza amewahimiza na kuwaomba wananchi, wakazi na madiwani wa maeneo mbalimbali waendelee kutoa ushirikiano kwa mkandarasi VETA  ili kuweza kukamilisha utekelezaji wa mpango wa anuani za makazi na postikodi kwa kutoa majina ya mitaa na idadi ya nyumba.

Miundombinu
Maoni