Rais Bush H.W aagwa kitaifa, watu maarufu watoa heshima zao

|
Rais mstaafu George W Bush na mkewe Laura wakati wa ibada ya mazishi ya mzazi wake aliyekuwa rais wa Marekani wa 41. George HW Bush Sr

Mwili wa rais wa zamani wa Marekani George H.W.Bush umeagwa mjini Washington na kufuatiwa na ibada ya kanisani tukio lililowaleta pamoja viongozi na watu mashuhuri mbalimbali duniani kuhudhuria shughuli za kuagwa kwa rais huyo wa 41 wa Marekani.

Shughuli ya kuandaa mazishi zimefanyika katika Kanisa Kuu mjini Washington kuashiria maombolezo ya kitaifa ya siku tatu huku watu mashuhuri pamoja na wananchi wa kawaida wa Marekani wakiendelea kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa chama cha Republican ambaye alishuhudia kipindi cha mpito cha  vita baridi na kufanikiwa kuongoza vita vya ghuba ya Uajemi hususan nchini Iraq na kurithiwa na Bill Clinton wa Chama cha Democrat ambaye alimshinda katika uchaguzi wa mwaka 1992.

Miongoni mwa viongozi waliowasili mapema katika shughuli za maandalizi ya mazishi ya Bush katika Kanisa Kuu ni pamoja na makamu wa rais wa zamani wa Marekani, Dick Cheney, waziri wa ulinzi wakati wa utawala wake Colin Powell na mwenyekiti wake wa zamani mnadhimu wa majeshi na mtangazaji wa zamani wa habari na mtandao wa NBC, Tom Brokaw.

Marais wanne wa zamani ambao ni hai ni miongoni mwa watu mashuhuri waliokwenda kwenye shughuli za mazishi akiwemo George W.Bush ambaye pia ni mtoto wake wa kiume na ndiye aliyesoma wasifu wa marehemu Bush . Pia Rais Donald Trump alihudhuria shughuli hiyo.

Wengine waliopangwa kuhudhuria ni Mfalme na Malkia wa Jordan, Wana wa Wafalme wa Uingereza na Bahrain, Kiongozi wa Ujerumani Angela Markel na Rais wa Poland ni miongoni mwa watu mashuhuri kutoka nchi mbalimbali duniani.

Bush, ambaye alihudumu kama rais wa 41 wa Marekani kati ya mwaka 1989 na 1993, amefariki dunia Ijumaa iliyopita akiwa na umri wa miaka 94.

Atazikwa nyumbani kwake Texas pembeni mwa kaburi la mkewe Barbara. 

Maisha
Maoni