Rais Kenyatta asaini Muswada wa sheria ya mitandaoni

|
Rais Uhuru Kenyetta

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameisaini Muswada wa Sheria za Uhalifu wa Kompyuta na Mtandaoni wa 2018 kuwa Sheria, hatua itakayotoa adhabu kali kwa watakaopatikana na makosa ya mitandaoni.

Sheria hiyo inatoa adhabu ya faini ya Shilingi milioni tano (5) za Kenya sawa na dola 50,000 za Marekani au kifungo cha miaka miwili jela au adhabu zote mbili kwa atakayepatikana na kosa la kueneza habari za uzushi.

Mtu atakayepatikana na kosa la kueneza taarifa ambazo zinaweza kuzua taharuki au kuzua vurugu atafungwa jela zaidi ya miaka kumi.

Sheria hiyo inatarajiwa kuathiri utendakazi wa wanahabari, vyombo vya habari, watumiaji wa mitandao ya kijamii, wanablogu na watu wengine wanaotumia kompyuta na mitandao.

Wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa wanahabari mapema mwezi huu, Mwenyekiti wa Chama cha Wahariri Kenya, Churchill Otieno alisema sheria hiyo inaweza kutumiwa kuminya uhuru wa wanahabari.

Alieleza kuwa kifungu kinachozungumzia uenezaji wa habari za uzushi au uongo kinaweza kutumiwa vibaya na maafisa wa dola.

Kiongozi wa zamani wa Chama cha Wanasheria Kenya, Apollo Mboya amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kifungu hicho kinaweza kuwapa watawala 'uhuru' wa kukandamiza vyombo vya habari.

Utawala
Maoni