Rais Magufuli awashukuru madaktari wa 'Save the child's Heart'

|
Rais John Magufuli akizungumza na madaktari wa 'SAVE THE CHILD'S LIFE' na wa Hospitali ya JKCI na MOI Ikulu jijini Dar es Salaam

Rais John Magufuli amewashukuru madaktari takribani 30 kutoka nchini Israel na Marekani ambao wamekuja nchini kwaajili ya kuokoa maisha ya watoto wa Kitanzania na kusema ndilo kusudi la kuwaita Ikulu kama njia ya kuwaonesha shukrani zake kwao.

Rais Magufuli ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokutana na wataalamu hao wa SAVE THE CHILD’S HEART walioambatana na wenzao wa Tanzania kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na MOI.

Rais Magufuli katika hotuba yake mbali na kuwashukuru wataalamu hao, amemwelekeza Naibu waziri wa Afya, Faustine Ndugulile kumfikishia shukrani zake kwa watoa huduma za afya nchini na kuwatia moyo, akiwataka wafanye kazi kwa moyo kwani anatambua kazi wanayoifanya na inafanya kila linalowezekana kutatua changamoto zilizopo.

"Nazijua changamoto mlizonazo, lakini hatuwezi kuzimaliza kwa siku moja, na ndiyo maana tunajitahidi kuongeza bajeti ya afya kila mwaka." alisema Rais Magufuli.

Amesema Serikali yake inajivua ushirikiano uliopo kati yake na mataifa mengine na kuwataka madaktari hao kuja nchi pia kama watalii badala ya kuja kufanya kazi tu.

Katika kuhimiza suala la utalii nchini, Rais Magufuli, amewapa ofa wataalamu hao ambao wanatarajiwa kukaa nchini hadi Novemba 10 kwenda kujionea vivutio vilivyopo mbugani na kupumzika huko kwa siku tatu iwapo wataridhia.

Rais Magufuli ameishukuru Israel kwa nafasi za mafunzo wanayowapa wataalamu wa ndani nchini mwao na kuomba kama idadi hiyo inaweza kuongezeka katika tasnia nyingine sanjari na kukaribisha wawekezaji wa vifaa tiba na dawa huku akiwahakikishia uwepo wa soko la uhakika nchini na nje ya nchi.

Rais Magufuli pia amemkabidhi Balozi wa Israel nchini, Barua ya shukrani aliyomwandikia Waziri mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyau, sambamba na kutoa zawadi kwa madaktari hao wa SAVE THE CHILD'S HEART na wa ndani pia.

Awali Naibu Waziri wa Afya, Faustine Ndugulile alisema, mpaka sasa Israel imefanikiwa kuwasomesha madaktari Saba pamoja na kuwapatia mafunzo wauguzi sita.

“Hii inadhibitisha kwamba badala ya kutupatia samaki, wao wanatufundisha kuvua ili kupunguza gharama za matibabu.” Alisema Naibu waziri.

“Hadi sasa tunapozungumza watoto takribani 60 walishatibiwa nchini Israel na kuendesha kambi takribani nne”

”Wagonjwa wanaotarajiwa kuonwa ni 50. Kwa upande wa gharama Ndugulile amesema, uwepo wa wataalamu hao nchini huokoa fedha nyingi kwani  iwapo wakipelekwa nje ya nchi wanatumia dola milioni 29 lakini wakitibiwa nchini wanagharimu dola 2000.

Afya
Maoni