Rais Paul Kagame apokea kijiti cha Museveni

|
Rais wa Rwanda, Paul Kagame akizungumza mara baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa EAC na Rais mwenza wa Uganda, Yoweri Museven

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenye mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi za EAC unaofanyika jijini Arusha akichukua nafasi ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Mkutano huo umehudhuriwa na marais kutoka, Tanzania, John Magufuli, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Makamu wa kwanza wa Rais wa Burundi na Mwakilishi kutoka Sudan Kusini.

Wakati huo huo, Jaji Sauda Mjasiri kutoka Tanzania amekula kiapo cha kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki katika mkutano uliofanyika jijini Arusha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi na wanafunzi walioshiriki shindano la insha la Afrika Mashariki ambapo washindi mbalimbali walikabidhiwa zawadi.

Akizungumza kwa kifupi mara baada ya kukabidhi nafasi hiyo, Kagame ameahidi kutumikia nafasi hiyo kwa kadri ya uwezo wake, na kushirikiana na wenzake kwa maendeleo ya ukanda wote wa Afrika Mashariki.

Mkutano huo wa 20 wa kawaida wa Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha Februari mosi ambapo masuala mbalimbali yamepitishwa kwa maendeleo ya Afrika Mashariki inayokadiriwa kuwa na watu takribani milioni 150.  

Utawala
Maoni