Rais Trump asusia kikao chake na viongozi wa Democrats

|
Rais Donald Trump wa Marekani

Rais Donald Trump jana alitoka nje ya chumba cha mazungumzo na viongozi wa Baraza la Congress waliokutana kujadili juu ya mpango wa kuidhinisha fedha za ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico ambao unapingwa na wapinzani kutoka Chama cha Democrats.

Trump akionyesha kukasirishwa na hatua hiyo ya wajumbe wa Democrats, aliandika katika ukurasa wake wa twitter kuwa ilikuwa ni kupoteza muda kwa kufanya mkutano na viongozi waandamizi wa Congress kutoka Democrats, ambao wameonyesha dhahiri kutounga mkono ujenzi wa ukuta huo ambao Trump ametetea kuwa na faida kubwa ya usalama kwa Wamarekani.

Pande zote mbili zilikubaliana kufanya mkutano huo uliomalizika ghafla baada ya kuanza, lakini hakuna wa kulaumiwa kutokana na tukio hilo.

Kwa mujibu wa watu wanaomuunga mkono Trump katika mkutano huo wamesema, Rais Trump alianza kwa kuwauliza viongozi wa Democratic kama wangekubaliana na kuidhinisha fedha kwa ajili ya mradi huo ambao viongozi wa upinzani walisema hawakubaliani na hapo hapo mkutano ulimalizika ghafla kwa rais kutoka nje.

Spika wa Democrat katika Baraza la Wawakilishi, Nancy Pelosi, alinyosha mkono katika mkutano huo na kupinga mradi wa ujenzi wa ukuta ambapo Makamu wa Rais, Mike Pence alisema kwa mara nyingine viongozi wa Democrat hawako tayari hata kujadiliana.

"Watu wengi wafanyakazi hawatapata malipo yao na hii ina maanisha nini katika maisha yao, watashindwa kulipia mikopo ya nyumba, kulipia pango la nyumba kulipia mikopo ya magari kulipia ada za watoto wao shuleni na mambo kadha wa kadha. Rais anaonekana kutotambua hilo."

"Ninachofikiria kinaweza kuumiza vichwa kwa wafanyakazi wa Serikali 800,000 na mamilioni ya Wamarekani na jawabu la yote haya linatoka kwa wajumbe wa Democrats ambao wanasema hawako tayari kujadiliana juu ya suala hili. "

Suala la ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Marekani na nchi jirani ya Mexico limekuwa likimshughulisha Rais Trump. Trump anataka kuidhinishiwa dola bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta huo ambao amesema utasaidia kuwazuia wahamiaji haramu hatari kwa usalama wa Marekani huku wengine wakiwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya na wafanyabiashara ya watu.

Democrats wanasema ukuta huo utakuwa na faida ndogo katika kukabiliana na matatizo halisi ya mpakani na kwamba msimamo mkali wa Trump sana sana umechochea mgogoro wa kibinadamu.

Katika Ikulu ya Marekani, Trump amewaambia waandishi wa habari kuwa endapo atashindwa kuufanikisha hilo, atatangaza hali ya hatari ya kitaifa, hatua ambayo inamwezesha kuachana na Baraza la Congress na kuchukua fedha za ujenzi wa ukuta kutoka jeshini.

Utawala
Maoni