RC Pwani ataka wizi wa vifaa kwenye mradi wa SGR ukomeshwe

|
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza makamanda wa mikoa mitatu na yule wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kujipanga kuhakikisha wanadhibiti uharifu unajitokeza kwenye mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaopita katika maeneo ya Soga, Ngerengere na Morogoro

Mkuu huyo wa mkoa pia amewaagiza makamanda hao akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesi na mwenzake wa Morogoro na Kisarawe kujipanga kwaajili ya msako huo mkubwa wa wizi wa vifaa ambao umekuwa ukifanywa katika mradi huo.

Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo leo, Jumanne alipokutana nao ofisini kwake Kibaha, Pwani baada ya kufanya mazungumzo nao ya namna ya kukomesha vitendo hivyo vya uhalifu katika maeneo hayo ambayo mradi huo unapita kwa sasa, unaojengwa na Kampuni ya Kituruki ya YAPI MERKEZI na kumshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro kwa kuwaunga mkono kuhusu kuendeshwa kwa msako huo.

Amewataka makamanda hao kwa kushirikiana na yule wa TRC kuwaonya wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu wakiwemo wafanyakazi wa mradi huo wanaoshirikiana na watu wa nje kuacha mara moja tabia hiyo huku akiweka bayana kuwa tayari baadhi yao walishakamatwa na kuhukumiwa kwenda jela lakini bado mchezo huo haujakoma.

Ametaja baadhi ya vifaa ambavyo vinaibwa zaidi katika mradi huo kuwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi kama Saruji, Nondo na vinginevyo pamoja na mafuta ya Dizeli jambo ambalo linarudisha nyuma kasi ya kazi inayoendelea pamoja na kuisababishia hasara serikali ambayo inatumia fedha nyingi kukamilisha mradi huo.

Kwa upande wa makamanda hao pamoja na Kamanda wa Kikosi Cha reli kilichopo Ngerengere wamesema, wamekutana na mkuu huyo wa Mkoa wa  Pwani kwaajili ya kumpatia taarifa ya mikakati waliyojiwekea katika kuwabaini wale wote wanaotaka kukwamisha jitihada za serikali kwa kuiba vifaa vya ujenzi wa Reli ya SGR.

Makamanda hao wamesema utekelezaji huo umekuja baada ya kupokea agizo la IGP Simon Sirro la kuwataka wakutane na kuweka mikakati ya kuhakikisha wanadhibiti uharifu unaojitokeza kwenye Mradi wa Reli ya SGR unaopita Soga, Ngerengere na Morogoro.

Uhalifu
Maoni