Rich Mavoko uso kwa uso na Diamond BASATA

|
Rich Mavoko uso kwa uso na Diamond BASATA

Baada ya kuwepo kwa malalamiko ambayo yalikuwa yakitupwa na msanii Rich Mavoko dhidi ya uongozi wa WCB, leo, Alhamisi wawili hao wamekutana ana kwa ana ili kujadili tofauti zao ambazo zimeletwa na kupishana kimaslahi katika ufanyaji wa kazi.

Hivi karibuni msanii Rich Mavoko alitangaza kujitoa katika kundi la WCB linaloongozwa na Diamond Platnumz kwa sababu ambazo alizianisha mwenyewe lakini kubwa zaidi ikiwa ni kunyonywa kwenye upande wa maslahi pamoja na kutokutimiziwa baadhi ya vitu ambavyo aliahidiwa kwenye mkataba wake.

Wiki iliyopita Sallam SK, Meneja wa Diamond alihojiwa katika kipindi cha ‘The Playlist’ kinachorushwa katika redio ya ‘Times FM’ na kusema kuwa Rich Mavoko bado ni msanii wa WCB kama mkataba wake unavyoonesha.

Na akizungumzia kuhusu suala la kunyonywa na kupewa baadhi ya stahiki za msingi kama wasanii wengine, Sallam alisema kuwa vyote hivyo Mavoko anavipata na mkataba wake hauna matatizo yoyote kama alivyokubaliana nao na kuusaini. Kwa hivi sasa wameachia suala la mkataba kufanyiwa uchunguzi na Basata.

“Hata Rich Mavoko alipewa gari, Rich ni mtu ambaye hataki kupost vitu vyake, lakini alikuja akapewa gari, sikumbuki alipewa gari ya aina gani lakini alipewa gari.” Alisema Sallam SK

Kwa upande wake leo hii, mmoja kati ya mameneja wa WCB (Mkubwa Fella) amesema kuwa hakuna tatizo lolote la kutisha kati ya Rich Mavoko na Wasafi, huku Dokii ambaye anasimama kama Meneja wa Mavoko amesema kuwa hakuna chuki kati yao kwa sababu wote ni wasanii na wanategemeana.

Kwa sasa, uamuzi wa BASATA ndio unaosubiriwa ili kufahamu ni kipi kilichoamuliwa baada ya kikao cha majadiliano kumalizika.

Muziki
Maoni