Serikali, Bharti Airtel waafikiana mazuri, JPM apongeza

|
Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi na Mwenyekiti wa Bharti Airtel, Sunil Mittal wakitiliana saini makubaliano ya kumaliza mvutano wa umiliki wa Kampuni ya Airtel Ikulu jijini Dar es Salaam

Rais John Magufuli amesema, kilichotokea leo ni ushindi kwa Tanzania, Airtel na Wawekezaji, kwa sababu wote wanahitajiana.

Rais Magufuli amesema iwapo Airtel ingekufa watu wengi wangeathirika kuanzia wafanyakazi, wauza vocha, wamama wanaofanya biashara ndogondogo katika ofisi hizo, wafanyabiashara pamoja na wengine waliokuwa wakijipatia fursa kupitia kampuni hiyo.

Amesema, muafaka huo ni mwanzo mpya wa biashara kati ya Tanzania na Airtel na wawekezaji sanjari na kusisitiza mapambano dhidi ya rushwa.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo, Jumanne aliposhuhudia Utiaji saini wa Makubaliano kati ya Serikali na Kampuni ya Bharti Airtel katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha akizungumzia kuhusu makubaliano yaliyofikiwa pamoja na mchango uliotangazwa na Mwenyekiti wa Bharti Airtel, Sunil Mittal wa Dola milioni moja, Rais Magufuli ameagiza fedha hiyo ipelekwe kujenga Hospitali mkoani Dodoma ambayo awali pia ilitengewa fedha zilizotakiwa kutumika kwenye Sherehe za Uhuru mwaka jana.

 Kuhusu mgawanyo wa Hisa za kampuni hiyo uliofikiwa Rais Magufuli amepongeza makubaliano hayo na kuongeza kuwa katika biashara makubaliano hayo ni ushindi wa pande zote na kumuhakikishia mwenyekiti huyo aliyeambatana na ujumbe wake kuwa hataruhusu biashara hiyo waliyokubaliana Tanzania kumiliki hisa asilimia 49 na Bharti  Airtel asilimia 51 kuendeshwa kwa hasara.

Kwa uapnde wake Mwenyekiti wa Bharti Airtel, Sunil amesema, makubaliano hayo yameweka historia mpya ya ushirikiano kwa pande zote kunufaika na kusisitiza kuwa kilichobakia ni utekelezaji wa makubaliano hayo ndani ya siku 30 na kumuomba Rais Magufuli kupitisha Baraka zake ili makubaliano hayo yatekelezwa kwa haraka ndani ya siku 30.

Naye Kiongozi wa makubaliano ya timu ya MAJADILIANO kutoka Tanzania, Profesa  Paramagamba Kabudi amesema, mazungumzo yao kati ya Serikali na Bharti Airtel yalienda vizuri licha ya kuwepo kwa ushindani na mabishano makubwa lakini hatimaye walifikia makubaliano ya ushindi wa kila upande.

 Kiongozi huyo ameyataja baadhi ya makubaliano hayo kuwa ni pamoja na Bharti Airtel kutoa bilioni moja kila mwezi kwa Serikali, Bodi ya wakurugenzi kuwa na wakurugenzi saba huku Serikali ikipewa mamlaka ya kumchagua mwenyekiti kutoka kwa wakurugenzi hao watatu huku Bharti wakitoa wakurugenzi wanne.

Makubaliano mengine ni Afisa Mkuu wa Ufundi atatakiwa kuteuliwa na Serikali katika nafasi za juu tatu za kampuni hiyo. Pia Bharti na Serikali wanataraji kuandaa upya kanuni, mikataba ya uendeshaji na utendaji wa Kampuni kwa lengo la kuziba mianya ya matumizi yasiyofaa.

Aidha makubaliano mengine ni  pande hizo mbili zitashirikiana katika kuongeza tija na ufanisi sanjari na  kutumia miundombinu iliyopo katika matumizi shiriki na Kampuni ya Simu ya Tanzania (TTCL) suala ambalo si la lazima.

Pia pande hizo mbili zimekubaliana kuhakikisha zinachukua hatua za pamoja kulinda maslahi ya kampuni  na kuiwezesha kuendeshwa kwa faida.

Bharti pia imekubali kutoa gawio la asilimia 25, kutoa shilingi bilioni moja kila mwezi kwa serikali  sambamba na kuchukua hatua ya kupunguza mzigo wa deni uliokuwa ukiisumbua Airtel.

Biashara
Maoni