Serikali yatoa onyo kwa wanaoingiza vyakula kiholela

|
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya wabunge Bungeni

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kuhakikisha zinachukua hatua kali dhidi ya watu wote watakaobainika wanaingiza nchini bidhaa za chakula na mafuta ya kupikia kwa njia za magendo.

Kadhalika, Waziri mkuu ameziagiza mamlaka husika kuhakikisha zinaendelea kudhibiti uingizwaji holela wa bidhaa mbalimbali za vyakula visivyokuwa na virutubisho yakiwemo mafuta ya kupikia na kutoa adhabu kali kwa wafanyabiashara watakaobainika kuingiza bidhaa hizo nchini.

Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo, Alhamisi, Novemba 15, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Vullu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alihoji kuhusiana na suala la uagizwaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje kama unazingatia sheria iliyopitishwa na Serikali ambayo inayolazimisha vyakula na mafuta ya kula kuwekwa virutubisho. 

Waziri mkuu amesema ipo sheria (Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219) inayohusu udhibiti wa vyakula yakiwemo mafuta ya kupikia ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na imeweka utaratibu wa kudhibiti uzalishaji, uagizaji, usambazaji pamoja na uhifadhi wa mafuta.

“Sheria hiyo pia inataka vyakula vyote vikiwemo vile vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi na vinavyozalishwa hapa nchini yakiwemo mafuta ya kupikia, lazima viwekewe virutubisho. Wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kulinda afya ya mlaji.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inakusudia kuanzisha kurugenzi au idara itakayosimamia fukwe zote nchini zikiwemo za bahari na maziwa  ili kuziimarisha na kuzifanya ziwe miongoni mwa vivutio vya utalii nchini.

Amesema kuimarishwa kwa fukwe hizo kutawezesha watalii kupata maeneo ya kupumzika mara wanapotoka kutembelea vivutio vingine vya utalii vilivyopo nchini kama mlima Kilimanjaro pamoja na mbuga mbalimbali za wanyama.

Waziri mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Kiteto Zawadi Koshuma aliyetaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza utalii nchini kupitia fukwe zilizopo katika ukanda wa bahari na maziwa ambazo zimeachwa bila kuendelezwa.

Wakati huo huo wabunge wanne waliopita bila kupingwa katika majimbo yao baada ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakitokea Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo wamekula kiapo Bungeni huku wakipokewa kwa shangwe na nderemo na wabunge wa CCM.

Wabunge hao ni James Ole Milya wa Simanjiro, Joseph Mkundi wa Ukerewe, Rioba Chacha wa Serengeti na Pauline Gekul wa Babati Mjini.

Chakula
Maoni