Serikali yawapa 'dili' wabanguaji korosho wa ndani

|
Miongoni mwa wabanguaji wa korosho wa ndani wanaoendelea na kazi hiyo

Serikali imeanza mchakato wa kuzibangua korosho ghafi ambapo imewaagiza wabanguaji wa ndani kuainisha mahitaji yao, uwezo na gharama ili waweze kuzibangua korosho hizo kwa niaba ya serikali huku ikitoa siku mbili kwa wabanguaji hao kukamilisha zoezi hilo.

Waziri wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amesema serikali imeamua kuvitumia viwanda vya ndani kubangua korosho zote ilizozinunua huku ikitoa siku mbili kwa wabanguaji hao kuainisha gharama, mahitaji na uwezo wao.

Kakunda amesema kuwa serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wa viwanda hivyo Serikali haitakubali kuhujumiwa inapoendelea kuboresha uwekezaji, uanzishaji na uendelezaji wa viwanda.

Alisema kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na upendo hivyo wafanyabiashara kote Duniani wana wajibu wa kujitokeza na kuanzisha biashara zao pasina kadhia yoyote.

Aliongeza kuwa mawakala wanaotumiwa kuvuruga uchumi wa viwanda na serikali kwa ujumla wake watachukuliwa hatua zinazopaswa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema jumla ya tani 275,000 zinatarajiwa kuvunwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2018/19 ambapo serikali imeamua kuwa kiwango hicho chote kitabanguliwa ndani ya nchi.

Jumla ya viwanda  vya kubangulia korosho nchi nzima  ni 23 ambapo kati ya hivyo viwanda 15 ni vibovu huku viwanda vinane pekee ndiyo vinavyofanya kazi vikiwa na uwezo wa kubangua tani 40,000.

Alisema wakati serikali inaendelea kukamilisha uhakiki wa wakulima wa korosho pamoja na kuendelea na malipo ya wakulima mpaka hivi sasa tayari wakulima 77,380 wamekwishalipwa hivyo hakuna korosho itakayoruhusiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi bila utaratibu maalumu badala yake korosho zote zitabanguliwa nchini.

Hasunga aliongeza kuwa Korosho zitakazoruhusiwa kwenda nje ya nchi ni zile tani 2000 pekee zilizonunuliwa mnadani na kampuni mbili kwa utaratibu uliokuwa ukitumika awali.

“Hakuna kampuni yoyote wala mfanyabiashara yoyote anayeruhusiwa kusafirisha korosho nje ya nchi baada ya tamko la serikali kutolewa” Alikaririwa Hasunga

“Tuwe na uwezo wa kubangua ama hakuna lakini korosho zote zitabanguliwa nchini, hivyo wito wangu kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya ubanguaji usiku na mchana” Alisema

Hasunga aliongeza kuwa serikali imeanza mchakato wa kuwafuatilia baadhi ya wafanyabiashara wenye uwezo wa kujenga viwanda kwa kufunga mitambo ndani ya muda mfupi.

Biashara
Maoni