Simba yarejea ligi kuu kwa kishindo, yaichapa Mwadui FC 3-0

|
Magoli yote ya Simba yamefungwa ndani ya dakika 10.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC leo wamerejea kwenye ligi hiyo kwa kishindo baada ya kuichapa Mwadui FC mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Magoli yote ya Simba yamefungwa ndani ya dakika 10 za kipindi cha kwanza wafungaji wakiwa ni Meddie Kagere dakika ya 21, Mzamiru Yassin dakika ya 26 na John Bocco dakika ya 29.  

Kwa matokeo hayo Simba imerejea kwenye nafasi ya tatu ikifikisha pointi 36 sawa na Lipuli FC nyuma ya Azam FC wenye pointi 48 huku vinara Yanga wakiwa na pointi 55.  

Katika mchezo mwingine uliopigwa leo Wagosi wa Kaya timu ya Coastal Union leo wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na Wazee wa Kupapas, Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

Wageni wa mchezo huo Ruvu Shooting ndiyo waliotangulia kupata bao kupitia kwa William Patrick dakika ya 37 kabla ya Coastal Union kusawazisha kupitia kwa Raizin Hafidh dakika ya 65. 

Coastal Union imefikisha pointi 30 na kukaa nafasi ya tisa baada ya kucheza mechi 23 huku Ruvu Shooting ikifikisha pointi 29 katika nafasi ya 12 kwa michezo 25 iliyocheza.

TPL
Maoni