Simiyu kuunusuru mkoa kuwa jangwa, waanza kupata miti
Mkoa wa Simiyu unatajwa kuwa na hali mbaya ya uoto kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo kukata miti kwa ajili ya matumizi ya nishati ambapo imeelezwa kwamba kwa mwaka mzima mkoa huo huzalisha magunia ya mkaa 100 kwa makadirio ya chini na kuni mita za ujazo 50.
Katika kukabiliana na hali hiyo taasisi ya Josephat Tonner imeanzisha Kampeni ya Simiyu ya kijani kwa kupanda miti maeneo ya wazi mkoani Simiyu.
Azam TV imeshuhudia kuanza kwa kampeni hiyo ikiwashirikiana vijana wa UVCCM Wilaya ya Bariadi ambao kwa pamoja na Taasisi ya Josephat Tonner imepanda miti 500 katika Mtaa wa Majengo wilayani humo.
Kaimu Meneja misitu wa wilaya hiyo ya Bariadi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Abdul Mohamed amesema Serikali Ina kazi kubwa ya kuelimisha jamii juu upandaji miti ili kurudisha hali ya uoto mkoani humo.
Taasisi hiyo ya Josephat Torner ni taasisi inayotetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi, imesema imeamua kuanza kampeni hiyo lengo likiwa ni kulinda mazingira yanayoweza kuleta athari kwa wenye ualbino ambao hukumbana na tatizo kubwa la ugonjwa wa saratani ya ngozi hivyo uwepo wa miti mingi husaidia kuleta vivuli.