Singapore nayo yazuia ndege za Boeing 737 max 8 kutua

|
Ndege aina ya Boeing 737 Max 8 zilizopigwa marufuku kutua katika viwanja vya ndege vya Asia

Nchi ya Singapore imeongezeka katika idadi ya nchi zilizozuia ndege aina ya Boeing 737 Max 8 kutumika katika viwanja vyake kama hatua ya awali ya kiusalama.

Mamlaka ya Anga ya Singapore imechukua uamuzi huo baada ya Ndege ya Boeing 737 Max 8 mali ya Shirika la Ndege la Ethiopia kupata ajali mwishoni mwa wiki na kuua watu wote 157 waliokuwamo ndani ya ndege hiyo.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha chini ya miezi sita kwa aina hiyo ya ndege kuanguka dakika chache baada ya kuruka.

Oktoba mwaka jana aina hiyo ya ndege ya Kampuni ya Lion Air ya nchini Indonesia ilianguka baharini na kuua watu wote 189 waliokuwemo safarini.

Mbali na Singapore, nchi nyingine zilizochukua uamuzi wa kuzuia matumizi ya ndege aina ya Boeing 737 Max 8 kutumika katika viwanja vyake ni China, Indonesia, Ethiopia na Visiwa vya Kaiman.

Biashara
Maoni