SUMATRA: Mabasi yatakayokosa kifuatilia mwendo hayatapewa leseni

|
Mabasi ya mikoani yakiwa katika mwendo kasi ambao sasa SUMATRA wamekuja na mwarobaini wake

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imethibitisha haitaruhusu utolewaji wa leseni kwa mabasi yasiyofungwa kifaa chenye mfumo wa kufuatilia mwenendo lengo likiwa ni kudhibiti mwendo kasi ili kupunguza ajali.

Wakati SUMATRA imetoa msimamo huo naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe ametaka madereva wataochezea mfumo huo kuhakikisha wanachukuliwa hatua.

SUMATRA imekuja na mfumo huu ikiwa ni moja ya juhudi za kukabiliana na madereva wanaokimbia kupita kiasi ambao mara kadhaa wamekuwa wakitajwa kusababisha ajali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Gilliard Ngewe amesema tayari mfumo huo ulishaanza kufungwa kwenye magari na wataendelea na utaratibu huo.

Waziri wa Ujenzi, amewataka SUMATRA kuwajibika kwa kuwachukulia hatua madereva watakaochezea mifumo hiyo huku Katibu Mkuu wa TABOA naye akigusia kuhusu gharama za mfumo huo ambazo amedai ni kubwa na kuiomba serikali kuliangalia upya suala hilo hususan kwa wenye mabasi mengi. Gharama za kifaa hicho kinachotakiwa kulipiwa kila mwezi ni takribani shilingi 60,000 kwa basi moja.

Takwimu za SUMATRA zinaonesha zaidi ya mabasi 2000 yameshafungwa mfumo huo unaotajwa kuwa mwarobaini wa kupunguza ajali za barabarani nchini.

Usafiri
Maoni