Takribani watu 40 wamekufa kwenye mafuriko Uganda

|
Mafuriko yaliyotokea nchini Uganda

Takribani watu 40 wamefariki dunia nchini Uganda baada ya kukumbwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa iliyoonyesha mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa zimesema watu wengi waliofariki dunia wilayani Bududa ni wale waliofukiwa na matope na mawe yaliyoporomoka kutoka katika Mlima Elgon.

Mamlaka katika Wilaya ya Bududa zinasema vikosi vya uokoaji vinaendelea na kazi ya kutafuta watu waliopotea katika maeneo hayo na kuna hofu ya kuongezeka kwa vifo zaidi.

Hofu hiyo  inatokana na ukweli kwamba siku ya mafuriko ilikuwa ni siku ya soko na hivyo watu walikuwa wengi zaidi kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Bududa.

Mvua hizo pia zimesababisha uharibifu wa makazi ya watu pamoja na miundombinu ya barabara na hata kufanya mawasiliano katika baadhi ya maeneo kuwa magumu kwa sasa.

Mwaka 2010 takribani watu 100 walifariki dunia katika tukio kama hilo katika wilaya hiyo ya Bududa.

Mafuriko
Maoni