Trump amwengua Tillerson katika baraza la mawaziri

|
Rais Trump alipokuwa akizungumza kabla ya kumtimua Tillerson

Katika panga pangua ya wateule wake, Rais Donald Trump kwa mara nyingine  amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri kwa kumtoa Rex Tillerson kutoka nafasi ya waziri wa mambo ya nje na kumteua Mike Pompeo aliyekuwa mkurugenzi wa CIA kuchukua nafasi ya Tillerson.

Trump amekuwa rais wa Marekani ambaye wateule wake hawana uhakika wa kudumu katika nafasi zao kama ilivyokuwa kwa marais waliomtangulia.

Nafasi ya Pompeo katika CIA itachukuliwa na Gina Haspel, ambaye alikuwa Naibu wa Pompeo kwenye shirika hilo la Ujasusi la Marekani.

Gina anakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa mkurugenzi wa CIA. Tillerson amerejea kutoka ziara yake barani Afrika ambayo ilifupishwa saa chache kabla ya Trump kutangaza mabadiliko hayo.

Hata hivyo Rais Trump hajatoa maelezo yoyote kufuatia mabadiliko hayo.

Akimshukuru Tillerson kwa njia ya mawasiliano ya twitter kwa huduma yake, Trump amesema waziri mpya wa mambo ya nje atafanya kazi nzuri. Tillerson, afisa mkuu wa zamani wa kampuni ya ExxonMobil, aliteuliwa kushika wadhifa wa waziri wa mambo ya nje mwaka mmoja uliopita.

Wizara ya mambo ya nje imesema Tillerson hakuzungumza na rais na alikuwa hajui sababu ya kutimuliwa kwake.

Naibu waziri wake, Steve Goldstein amesema Tillerson alikuwa na nia ya kuendelea kuhudumu katika wizara hiyo kutokana na hatua iliyopigwa katika usalama wa taifa.

Lakini Tillerson ni nani hasa?

Rex Wayne Tillerson ni mwanadiplomasia wa Marekani na mwenye taaluma ya uhandisi wa majengo. Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini na pia ni afisa wa serikali wa 69 kushika wadhifa wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani. Aliteuliwa Februari Mosi, 2017 chini ya Rais Donald Trump.

Tilerson mmoja wa wanadiplomasia maarufu nchini Marekani na hivi karibuni alikuwa barani Afrika ambapo ametembelea nchi kadhaa zikiwemo Nigeria, Chad na  Kenya, ambako aliwapongeza Rais Uhuru Kenyatta na raila Odinga kwa kukutana na kuzungumzia maslahi ya taifa hilo.

Utawala
Maoni