TUCTA yaibua mjadala mpya wa mafao ya pensheni

|
Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya akizungumza na waandishi wa habari

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeibua mjadala mpya wa mafao ya Pensheni za wastaafu baada ya kutoa tamko la kupinga kikokotoo cha mafao hayo.

Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya amesema hayo leo Alhamisi, Disemba 6 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu utaratibu uliotumika, Rais huyo amesema, hawakukubaliana kabisa na namna ukokotoaji wa 1/580 na miaka 12.5 ya kuishi baada ya kustaafu ilivyofanyika katika hatua za awali za ukokotoo katika ushirikishwaji wa wadau.

Nyamhokya ameongeza kuwa kwa sasa uamuzi wa nini watafanya wanaurudisha kwa wafanyakazi, huku wakiiomba Serikali kuangalia upya na wanaimani watakapokutana na waziri mwenye dhamana ya ajira na kazi, watafikia muafaka mzuri na wenye unafuu na utakaoondoa kilio kilichopo na vijavyo.

Amesema namna mamlaka husika ilivyokokotoo mafao hayo ni wazi yatawaumiza wafanyakazi wa hali ya chini.

Hivi karibuni Serikali iliwasilisha Sheria mpya ya Mafao ya mwaka 2017 ambayo yalipitishwa na Bunge na hivyo kuzua malalamiko kila kona ikiwemo sheria ya mstaafu sasa kutoruhusiwa kuchukua fedha yake ya mfuko wa jamii aliyoichanga kwa kipindi chote cha utumishi wake kwa mkupuo na badala yake atatakiwa kuchukua asilimi 25 ya awali na 75 atakuwa akipatiwa kama mshahara wa mwezi.

Fedha
Maoni