Ubovu wa miundombinu ndani ya hifadhi wapatiwa ufumbuzi

|
Watalii wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro ambao hukumbana na ubovu wa miundombinu ndani ya hifadhi

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetenga zaidi ya shilingi bilioni 11 kwa ajili ya ujenzi wa barabara itakayotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya matofali maalumu kuanzia Lango Kuu la kuingia ndani ya Hifadhi hiyo LODWALE hadi kwenye Lango la Kuingia Hifadhi ya Serengeti GOLINI itakayokuwa na urefu wa Kilometa 88.

Mamlaka hiyo imesema, kusudi la ujenzi wa barabara hiyo ndani ya hifadhi ni kuondoa malalamiko kutoka kwa watalii na watoa huduma hizo kuhusiana na uchakavu wa miundombinu ya barabara za udongo ndani ya hifadhi.

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorongoro, Dkt. Fredy Manongi akizungumza na wanahabari kwenye ofisi zake zilizopo ndani ya hifadhi hiyo amesema tayari Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) pamoja na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wameridhia kujengwa kwa barabara hiyo.

Kwa upande wake Fundi Sanifu wa Mamlaka hiyo, Shabani Felician ameongeza kwamba kila mwaka Mamlaka hutumia zaidi ya shilingi bilioni Tatu (3) hadi Tano (5) kwaajili ya kutengeneza barabara zilizopo ndani ya hifadhi na ujenzi wa barabara hiyo mpya utasaidia kuokoa fedha hizo.

Mchakato wa ujenzi wa barabara tofauti na ile ya udongo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro umeonekana kuchukua muda mrefu kutokana na kukinzana kwa misimamo baina ya wadau wa sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi na kukubalika kwa jambo hilo kunaonekana kama ushindi mkubwa kwa wale waliokuwa wakilipigia upatu jambo hilo.

Miundombinu
Maoni