Uhamiaji: Waandishi wa CPJ walikiuka masharti ya viza

|
Waandishi Angela Quintal, Raia wa Afrika Kusini (kulia) na Muthoki Mumo, Raia wa Kenya (kushoto),waliokuwa wamekamatwa na baadaye kuachiwajijini Dar es Salaam

Idara ya Uhamiaji Tanzania imethibitisha kuwakamata na kuwahoji Waandishi wa habari kutoka Kamati Maalum ya Kuwatetea waandishi wa habari Duniani (CPJ) na kisha kuwaachia huru kwa madai ya kukiuka masharti ya viza.

Akizungumzia suala hilo lililobeba vichwa vya habari na kusambaa katika mitandao ya kijamii ya ndani na nje ya nchi, Msemaji wa Idara hiyo, Mrakibu Ally Mtanda amesema, ni kweli waliwashikilia waandishi hao waliokuwa katika Hoteli ya Southern Sun baada ya kubaini waliingia nchini wakiwa na viza ya matembezi lakini wamekuwa wakijihusisha na mahojiano na waandishi wa habari.

Mtanda amesema, waandishi hao Angela Quintal Raia wa Afrika Kusini na Muthoki Mumo, Raia wa Kenya, waliingia nchini Oktoba 31 kwa viza ya matembezi ya kawaida lakini baadaye walibaini wawili hao ambao viza zao zinaishia Januari mwakani walikuwa wakienda kinyume na madhumuni ya viza hizo.

“Idara yetu haiishii tu kwenye kutoa viza bali huwa tunafuatilia kama muhusika anafuata masharti aliyopewa katika viza, kwa kuendana na madhumuni aliyoyaainisha awali ya kuingia nchini,” alisema Mtanda

Mtanda amesema baada ya kuwashikilia kwa muda, waliwaelekeza na kuwafundisha wanachopaswa kufanya kuendana na masharti ya viza yao kwa sababu kama walikuwa na lengo la kufanya mikutano na waandishi wa habari, basi walipaswa kuwasiliana na Idara ya Habari Maelezo na mamlaka zinazohusika kabla ya kuanza kufanya shughuli hizo.

Utawala
Maoni