Uingereza yaijaza Tanzania 'Mahela'

|
Rais Magufuli akimpokea Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Penny Mordaunt Ikulu Jijini Dar es Salaam

Uingereza imetoa msaada wa shilingi bilioni 307.5 kwa Tanzania kwaajili ya kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya.

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Penny Mordaunt ametangaza kutoa msaada huo leo, Ijumaa Agosti,10 alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Penny Mordaunt amesema, fedha hizo zinatolewa kwaajili ya kuunga mkono vipaumbele vya Rais Magufuli ambapo kati yake shilingi bilioni 124.5 zitaelekezwa katika kuinua ubora wa elimu hususani kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu, shilingi bilioni 23.5 zitaelekezwa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa na shilingi bilioni 160 zitaelekezwa katika kuboresha huduma za afya.

“Tunafanya hivi ili kudhihirisha dhamira yetu ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu, tunataka kujielekeza katika kuhakikisha Mhe. Rais Magufuli anafanikisha ahadi zake kwa Watanzania na tunafurahi kuwa wadau muhimu wa hilo” alisema Penny Mordaunt.

Waziri huyo ameongeza kuwa pamoja na kuwa wachangiaji wakubwa katika bajeti ya Serikali, Uingereza ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania na kwamba wanafurahishwa na wito wa Rais Magufuli kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara zaidi kutoka Uingereza watakaowekeza kwa manufaa ya pande zote (win-win).

Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru waziri Penny Mordaunt kwa msaada huo na amemuomba kufikisha shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kwa mchango mkubwa ambao Uingereza hutoa kuchangia bajeti ya Serikali na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Namshukuru sana Waziri Penny Mordaunt kwa kutambua juhudi zetu za kuinua elimu, kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuboresha huduma za afya, msaada huu utatusaidia kuongeza nguvu kwa sababu watoto wakipata elimu bora, tukikomesha rushwa na watu wetu wakiwa na afya njema tutaweza kujenga viwanda na kukuza uchumi wetu kwa kasi zaidi” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amemuahidi Penny Mordaunt kuwa fedha zilizotolewa zitatumika vizuri na kwamba Serikali itahakikisha uhusiano wa Tanzania na Uingereza unazidi kuimarishwa kwa kuwa inatambua Uingereza ndio mwekezaji mkubwa nchini na imekuwa ikitoa misaada mikubwa ya fedha za walipa kodi wa Uingereza kwaajili ya maendeleo ya Tanzania.

Pia, Rais Magufuli amemkabidhi Penny Mordaunt albamu ya picha za shule ya sekondari Ihungo mkoani Kagera iliyojengwa upya baada ya kuharibika vibaya kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 2016, na ameishukuru Uingereza kwa msaada wa shilingi bilioni sita (6) zilizotumika kujenga majengo hayo kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dkt. Augustine Mahiga ambaye amesema ziara ya Waziri Penny Mordaunt imezidi kukuza uhusiano wa Tanzania na Uingereza.

Utawala
Maoni