Viongozi Afrika wakubaliana kukabili ongezeko la vijana

|
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano wa viongozi wa Afrika ulifanyika nchini Uganda

Viongozi wa Afrika wamekubaliana kuwepo kwa ongezeko la idadi ya Vijana barani humo jambo ambalo limekuwa likisababisha kuwepo kwa changamoto kadhaa wa kadhaa kwenye mataifa husika.

Kutokana na ongezeko hilo viongozi hao wameona ni vyema kukawa na mkakati wa kuwahusisha kutoa elimu ya kuwawezesha kujiajiri lakini kazi kubwa ikiangaliwa kwenye ukuzaji wa uchumi wa mataifa hayo.

Hayo yameafikiwa leo, katika mkutano wa siku mbili wa Africa Now uliofanyika nchini Uganda Tanzania imewakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais John Magufuli.

Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na changamoto hiyo wakati huu ndiyo unawapasa viongozi wa Afrika kuiangalia Afrika ijayo na viongozi wa sasa hawana budi kuandaa mazingira ya Afrika bora na salama.

Makamu wa Rais amesema mkutano huo umeangalia suala zima la ongezeko la watu na uelewa wa vijana katika maendeleo ya nchi zao hususan wakati huu ambapo nchi nyingi zinajipambanua katika uchumi wa viwanda na kuhimiza suala la kuangalia mitaala ya elimu inayotolewa sasa kama inakidhi mahitaji ya kisayansi na kiteknolojia.

“Lazima sasa tuangalie hii idadi ya watu isije ikawa chanzo cha kuleta vurugu katika nchi zetu bali iwe chanjo cha nguvu kazi kujenga nchi zetu,”alisema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Afrika ya sasa inahitaji Viongozi ambao hawajitazami wao bali wanatazama wananchi wao katika makundi yao kama Vijana, Wanawake na Walemavu.

Makamu wa Rais pia alikutana na kuzungumza na Naibu Rais wa Kenya, William Ruto ambapo baada ya kikao hicho Makamu wa Rais amesema Tanzania na Kenya ni majirani pamoja na kuwa kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki lakini wao kama nchi jirani lazima wahakikishe uhusiano wao unasimama imara na kukuza ushirikiano.

Utawala
Maoni