Viongozi Saba wa CHADEMA wafikishwa mahakamani Kisutu

|
Wabunge wa CHADEMA waliofikishwa mahakamani leo, Jumatatu

Kesi inayowakabili Viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inatarajiwa kuendelea kesho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar Es Salaam ambapo leo Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya ameunganishwa katika kesi.

Bulaya ameunganishwa katika kesi hiyo akiwa na shtaka la kumi na mbili la kushawishi kutenda kosa la jinai ambapo inadaiwa February 16, mwaka huu katika Viwanja vya Buibui aliwashawishi wakazi wa Kinondoni kufanya maandamano yenye vurugu.

Kesi hiyo itaendelea kesho baada ya leo upande wa mashtaka kuomba muda zaidi ili wajiandae kujibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi unaotaka kuanzia shtaka la nne hadi la tisa litolewe ufafanuzi na Mahakama Kuu kama yanastahili kuwa jinai.

Bulaya amekana mashtaka yanayomkabili ambapo upande wa mashtaka wamedai kuwa upelelezi umekamilika na hivyo ameunganishwa kwenye kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkuu Wilbard Mashauri ambapo upande wa mashtaka unawakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Peter Kibatala

Kabla ya mshtakiwa kusomewa maelezo yake wakili wa upande wa utetezi Kibatala aliomba mteja wao kupatiwa dhamana kwa masharti kama ya wenzake ambapo hakimu aliridhia maombi hayo huku akitoa masharti ikiwa ni pamoja na masharti kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya milioni 20 kila mmoja lakini pia kila mmoja awe na barua ya utambulisho mshtakiwa amepata dhamana mara baada ya kutimiza masharti ya dhamani huku akitakiwa kuripoti kituo cha polisi kila ijumaa

Kabla ya mshtakiwa kupatiwa dhamana upande wa utetezi uliwasilisha hoja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuomba Mahakama ya Kisutu kuridhia shtaka la nne hadi la tisa kupelekwa katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kupatiwa ufafanuzi juu ya jinai kwa kile wanachodai kuwa watu kutoa maoni yao kuhusu mwenendo wa nchi ni haki yao na si kosa.

Wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi amesema hoja zote zilizowasilishwa na upande wa utetezi hazina mashiko hivyo anaomba kuzijibu Aprili 17, mwaka huu saa mbili asubuhi.

Aidha washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni pamoja na mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu katibu mkuu Bara, Peter Mnyika, Salum Mwalimu, Estar Matiko, Katibu mkuu wa chama hicho Dkt. Vincent Mashinji pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

 

 

Mahakamani
Maoni