Viwanda vya ndani vyakabidhiwa kazi ya kubangua korosho

|
Baadhi ya watendaji wa viwanda vilivyopewa jukumu la kubangua korosho wakisaini makubaliano waliyoafikiana na serikali

Serikali imetiliana saini makubaliano ya kuanza kubangua korosho na Kampuni manne yanayomiliki viwanda vya  ubangujia ili vianze kubangua zao hilo ambapo katika hatua ya awali jumla ya tani 7,500 zinatarajiwa kubanguliwa huku wito ukitolewa kwa kampuni nyingine kujitokeza kufanya kazi hiyo.

Hatua hiyo imeshuhudiwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga jana, Januari 10 mkoani Mtwara ambapo wahusika wakuu walikuwa ni Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania na wenye viwanda vya ndani.

Mara baada ya utiaji saini huo, Waziri Hasunga amesema hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuzuia usafirishaji wa korosho ghafi nje ya nchi na kuagiza korosho zote zibanguliwe nchini.

Mkurugenzi wa Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania, Dkt Hussein Mansoor  ndiye aliyeiwakilisha serikali katika utiaji saini  na Kampuni hizo nne ambazo ni Kampuni ya Hawte Investment Co. Ltd, Micronix Mtwara, Korosho Afrika na Micronix- Newala.

Kampuni hizo zimeingia mikataba ya Jumla ya Tani 7500 ambapo kampuni ya Hawte Investment Co. Ltd ina uwezo wa kubangua Tani 2000 kwa mwaka na imesaini mkataba wa kubangua tani 1,500.

Kampuni ya Micronix ya mjini Mtwara yenye uwezo wa kubangua tani 2,400 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua tani 1,200. Kampuni ya Korosho Afrika ya Mjini Tunduru mkoani Ruvuma yenye uwezo wa kubangua tani 5,000 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua tani 2,400 ilhali Kampuni ya Micronix ya wilayani Newala yenye uwezo wa kubangu tani 5000 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua tani 2,400.

Aidha Waziri Hasunga  amesema kuwa Serikali imepitia vifungu vyote vya kisheria kabla ya kuanza kuingia makubaliano na kampuni hizo kwa ajili ya ubanguaji wa Korosho.

Biashara
Maoni