Waajiri waliokusanya madeni ya HESLB wapongezwa

|
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akikabidhi ngao kwa mmoja wa waajiri waliotambuliwa na Bodi ya Mikopo kwa kusaidia kukusanya madeni kwa wanufaika

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imewatambua waajiri wanaofanya vyema kwenye ukusanyaji wa fedha za mikopo kwa waajiriwa walionufaika na huduma hiyo kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwa kuwakabidhi ngao kama alama ya kuwapongeza kwa ushirikiano wao.

Katika utekelezaji wa majukumu yake Sheria imeipa bodi hiyo jukumu la kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu walionufaika na mikopo hiyo kuanzia mwa 1994 ili fedha hizo zitumike kukopeshwa wanafunzi wengine.

Zoezi la kuwatambua waajiri hao limefanyika Jijini Arusha ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Abdul-Rarak Badru ameeleza kwamba kwa mwaka 2017/2018 kwa nchi nzima makusanyo yalifikia shilingi bilioni 181.

Katika Mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Arusha licha ya kuhimiza waajiri kutilia mkazo suala la ukusanyaji na urejeshaji wa mikopo kutoka kwa waajiriwa wake ametoa rai kwa bodi hiyo pia kutazama upya mpango unaoonekana kuwaweka kando wanafunzi waliopitia shule za binafsi kwa madai wazazi wao wana uwezo wa kuwaendeleza katika elimu ya juu na hivyo kukosa mikopo.

Bodi ya mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba 9 ya mwaka 2004 na ilianza kazi mnamo mwezi Julai 2005.

Elimu
Maoni