Waandamana kushiniza shule ya Rubondo ifunguliwe

|
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki maandamano na wazazi wao kushinikiza shule mpya kufunguliwa

Wazazi na Walezi katika Kitongoji cha Mchangani katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa na watoto wao ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Ihumilo na Mwaloni wameandamana hadi kwenye Shule Mpya ya Rubondo wakiushinikiza uongozi wa kuifungua shule hiyo ili watoto wa Darasa la awali, la kwanza na la pili wasome shuleni hapo kwa lengo la kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita tatu kwenda shuleni.

Kufuatia maandamano hayo, wanafunzi zaidi ya 600 wa kitongoji hicho hawakuweza kuhudhuria masomo darasani na badala yake waliungana na wazazi wao kisha kuhitimisha maandamano hayo kwenye Shule hiyo ya Msingi Rubondo ambayo bado haijafunguliwa na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa ngazi ya kata.

Wakizungumza mara baada ya kufika kwa viongozi wa kata hiyo, wazazi na watoto hao wameitaka serikali kuifungua shule hiyo ili watoto wao waweze kusomea vyumba vilivyopo badala ya kuvifunga ili kuwapunguzia safari watoto hao pamoja kuepusha na ajali za mara kwa mara zinazopoteza maisha ya wengi.

Hata hivyo, akizungumza na umati huo, mktendaji wa kata amewaahidi wazazi na watoto hao kuifungua shule hiyo sanjari na kuwahimiza kukamilisha vyoo vya wanafunzi na walimu kazi ambayo amesema itafanyika haraka iwezekanavyo.

Hatua hiyo inakuja kufuatia kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya ajali za barabarani ambapo mwishoni mwa juma lililopita mwanafunzi Denice Cleophace wa darasa la Pili alifariki dunia baada ya kugongwa na pikipiki akitoka shule.

Elimu
Maoni