Waandishi wanawake 80 kutoka barani Afrika waitikisa Naivasha

|
Wanawake waandishi wa habari waliokusanya mjini Naivasha, Kenya kwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiuongozi na kiteknolojia

Katika kuhakikisha wanawake kutoka vyombo mbalimbali vya habari barani Afrika wanakuwa na uwezo na weledi katika kuongoza vyumba vya habari, taasisi za kimataifa zinazohusika na masuala ya kuwajengea uwezo wanawake zinawakutanisha wanawake takribani 80 mjini Naivasha, Nakuru huko Kenya.

Wanawake hao kutoka nchi zaidi ya 10 walikutana katika Hoteli ya Great Rift Valley, ambapo pamoja na mambo mengine, walipata nafasi ya kubadilishana uzoefu sambamba na kujadili masuala mbalimbali yanayowakabili kwenye kazi zao ndani ya vyumba vya habari.

Miongoni mwa mafunzo yaliyotolewa na wakufunzi waliobobea katika tasnia ya habari ni pamoja na yale ya Uandishi wa habari kwa kutumia simu ya mkononi, (Mobile Journalism) yaliyotolewa na mbobezi wa masuala ya digitali nchini Kenya, Churchill Otieni ambaye alisisitiza umuhimu wa kupiga picha zinazoeleza habari kikamilifu sanjari na masuala ya usalama na matumizi sahihi ya mawasiliano ya simu.

Aidha kwa upande wa mkufunzi Jane Godia kutoka Kenya aliwafumbua macho wanawake hao waandishi  kwa kuwaeleza tafsiri na aina za udhalilishaji zinazowakabili wengi wao kwenye vyumba vya habari sanjari na namna ya kujiepusha ama kujinasua katika sauala hilo.

Mbali na mafunzo ya Utawala na uongozi , Usalama wa mazingira hatarishi kazini na maeneo mengine ya kazi, wakufunzi hao wabobezi pia kupitia Taasisi ya Kimataifa ya Mfuko wa Waandishi wa Habari wanawake (IWMF) walioshirikiana na Women in News (WIN) waliendesha pia mafunzo ya uandishi wa Takwimu na yale ya utengenezaji vipindi vya sauti kupitia simu za mkononi maarufu (podcasting).

Wanawake hao kutoka Barani Afrika ikiwemo Tanzania walitoka na kauli moja ya kuwa mabalozi katika vyumba vyao vya habari sanjari na kubadili utamaduni wa kufanyakazi kwa mazoea.

Pamoja na kufundishwa masuala hayo ya matumizi sahihi ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii, mbinu za kujikinga kwenye mazingira hatarishi, na upigaji wa picha zenye mvuto, wanawake hao pia walipata nafasi ya kuzungumza na wakongwe katika tasnia ya habari kwa lengo la kupata shuhuda na uzoefu wao kazini.

Waandishi hao wanawake kutoka nchi hizo akiwemo Cynthia kutoka Kenya, Sheila Ponnie wa Sudan ya kusini na Agnes Shayo kutoka Tanzania ambao kwa niaba ya wengine wamewashukuru IWMF na WIN kwa fursa na mafunzo waliyoyapata na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote waliyoyapata.

Tukio
Maoni