Wafundishwa kuthamini utunzaji mazingira na wanyama

|
Wanafunzi waliobahatika kupatiwa mafunzo ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori

Baadhi ya jamii zinazoishi kando kando mwa hifadhi zipo kwenye mpango wa makusudi wa kuongezewa uelewa na kuthamini mchango wa utunzaji wa mazingira na wanyamapori.

Mpango huo unaowalenga zaidi vijana unaratibiwa na Shirika la Kidunia la Hifadhi ya Mazingira liitwalo NATURE CONSERVANCY la nchini Marekani.

Utaratibu huu unatokana na kile kinachotajwa kutoweka kwa kasi kwa uoto wa asili huku Wanyamapori wakitoka katika hifadhi na kuingia kwenye maeneo ya vijiji wakiwa kwenye hatari ya kuuawa ama kujeruhiwa vibaya.

Utoaji wa elimu ya Hifadhi ya Mazingira umekuwa ukitolewa kwa mbinu mbalimbali kwa mfano katika Shule ya Msingi Njia panda iliyopo wilayani Karatu mkoani Arusha, jopo la wataalamu wa uhifadhi kutoka NATURE  CONSERVANCY ambao wanatoka nchi mbalimbali wameendesha zoezi la upandaji wa miti pamoja na ukarabati wa vyumba vya madarasa.

 

Chira Schouten mmoja wa wawakilishi wa NATURE CONSERVANCY nchini amesema kwa kufanya hivyo kunawajenga vijana walio shuleni uelewa wa kuwa Mazingira na Wanyama ni sehemu muhimu ya maisha.

Kwa upande wa uongozi wa Shule ya Msingi Njiapanda umesema kutokana na eneo hilo kupakana na Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro wanyama wengi wamekuwa wakitoka  hifadhini na kuingia vijijini na hivyo kwa kuwafunza watoto kuhusu uhifadhi kutawasaidia kufahamu mbinu mbalimbali zikiwemo kutokuwadhuru wanyama sambamba na serikali kupata mapato kupitia utalii.

NATURE  CONSERVANCY iliyotapakaa duniani kote , makao makuu yake yapo jijini  Washington DC, Marekani.

Utalii
Maoni