Wagoma kutaja watuhumiwa wa mauaji mbele ya RC

|
Mmoja wa wakazi wa Lamada akitoa maelezo ya kwanini hawatataja watuhumiwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu

Wakazi wa Kata ya Lamadi, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wameshindwa kuwataja watuhumiwa wa matukio ya mauaji ya watoto yanayotokea katika eneo hilo.

Wameshindwa kufanya hivyo mbele ya Mkuu wa Mkoa, Antony Mataka kwa madai ya kuhofia usalama wao.

Wakiwa katika mkutano wa hadhara kujadili njia za kukabiliana na mauaji hayo wakazi hao walilituhumu jeshi la polisi kwa kutotekeleza majukumu yao na kudai kuwa wengi wao wanashirikiana na wahalifu hao na wanawafahamu.

Takribani watoto watatu wameripotiwa kukutwa wakiwa wamekufa kwa kipindi cha miezi mitano ambapo watoto wote hupotea na baadaye kukutwa wamefariki dunia kwenye nyumba zisizokwisha (mapagale) au vichanga.

Baada ya kikao cha takribani saa nne mkuu huyo wa mkoa aliwataka polisi kujitafakari kutokana na hali halisi huku akiwashutumu maaskari wapelelezi kwa kuzembea kuwapata watuhumiwa na kuwahoji kwanini wasiondoke katika eneo hilo kwa kushindwa kazi na kuja wengine.

Mkuu wa mkoa huyo hata hivyo aliwataka wananchi hao kuendesha zoezi hilo kwa siri badala ya utaratibu wa awali na kuahidi kufika kwa ajili ya zoezi hilo, kesho kutwa Alhamisi.

Watoto waliuawa ni pamoja na Suzana Shija mwenye umri wa miaka tisa (9) aliyeuawa  Octoba 10, Milembe Maduhu miaka 12 aliyeuawa Januari 13 na Joyce Joseph miaka nane aliyeuawa  Februari 8, 2019.

Mauaji
Maoni