Wajelajela Tanzania Prisons waendeleza ushindi Sokoine

|
Wachezaji wa Tanzania Prisons wakishangilia goli lao pekee.

Maafande wa Jeshi la Magereza Tanzania Prisons wameendeleza wimbi la ushindi kwenye uwanja wa nyumbani baada ya kuwatembeza kwata wapiga debe kutoka Shinyanga Stand United kwa bao 1-0.

Huu ni mchezo wa tatu mfululizo maafande hao wakiibuka na ushindi wa pointi tatu kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya.

Mwishoni mwa wiki iliyopita wajelajela hao waliwafunga Mbao FC kutoka jijini Mwanza mabao 2-1 na kupanda hadi nafasi ya 17.

Alikuwa ni mshambuliaji wa kati Adam Adam aliyeipatia timu yake goli pekee mnamo dakika ya 50 ikiwa ni dakika tano tu tangu kuanza kipindi cha pili.

Adam alipachika goli hilo akipokea pasi toka kwa Benjamini Asukile na kuimalizia wavuni na kumwacha mlinda mlango wa wapiga debe hao Mohamed Makaka akichupa bila mafanikio.

Kwa matokeo hayo Prisons wamepanda nafasi moja hadi 16 wakiwa na alama 26 wakati Stand United wakibaki nafasi ya 13 wakiwa na alama 29.

TPL
Maoni