Wanamichezo 58 kuiwakilisha Tanzania michezo ya Afrika Mashariki

|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Susan Mlawi amewaaga wachezaji wa timu zinazokwenda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Burundi.

Wanamichezo 58 wa timu ya Tanzania itakayoshiriki michezo ya kwanza ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itakayofanyika nchini Burundi kuanzia Agosti 16 mwaka huu wameagwa rasmi leo katika hafla ya kukabidhiwa bendera iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika sherehe hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Suzan Mlawi, amewataka wanamichezo hao kwenda na kuipigania nchi huku wakiweka nidhamu na uzalendo mbele.

“Kwa sababu mashindano haya ni ya mara ya kwanza, naamini jina la Tanzania litabebwa,” amesisitiza Mlawi.

Mmoja wa makocha kutoka timu ya soka ya wanawake, Hababuu Ally amesema ana matumaini na kikosi cha timu hiyo ambacho kinaundwa na asilimia kubwa ya nyota waliotumika katika kikosi cha Kilimanjaro Queens kilichotwaa ubingwa wa CECAFA mwaka huu.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, Mwanahamis Omar amewataka Watanzania kutokuwa na shaka juu ya wachezaji hao, kwani wote wana maandalizi ya kutosha, hivyo wana uhakika wa kufanya vyema katika michuano hiyo.

Msafara huo wa watu 58 walioondoka leo kwa basi la timu ya Taifa Stars, unajumuhisha maafisa wanne wa serikali, wanariadha 10, wachezaji soka 23, wacheza karate 7 na wachezaji wa netiboli 14.

Michezo
Maoni