Wananchi Masienda walilia uchunguzi matumizi mabaya ya fedha

|
Shule ya sekondari Masieda ambayo iko Mbulu iliyojengwa kwa michango ya wananchi lakini sasa imekwama na hivyo kudai uchunguzi ufanyike

Wananchi wa Kata ya Masieda Wilaya ya Mbulu, Mkoa wa Manyara wameiomba Serikali ya Kijiji cha Masieda kufanyia uchunguzi juu ya matumizi mabaya ya fedha iliyochangwa na wananchi kwa zaidi ya mara nne, kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Masieda iliyolenga kuwaepusha watoto wao kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Michango hiyo ya wananchi kutoka Kata ya Masieda yenye wakazi 8,400 na kaya 1,350 ni tofauti na mchango wa bati 230 zilizotolewa na Mbunge wa Mbulu vijijini, Flatey Maasay alizotoa kwa ajili ya upauzi wa majengo ambayo yanalenga kuokoa watoto wa maeneo ya Masieda kutembea umbali wa kati ya kilomita 28 hadi 30 kwa mujibu afisa mtendaji wa kata hii.

Uchelewaji wa ukamilikaji wa ujenzi wa shule hiyo unatajwa kuendelea kuwaweka wanafunzi kutoka Masieda katika mazingira magumu kufikia malengo yao kielimu kutokana na umbali wanaotembea kufikia shule ya sekondari Gunyoda iliyopo katika Jimbo la Mbulu mjini.

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako aliwahi kutembelea shule hiyo na kuahidi kwamba serikali haitaruhusu kufunguliwa kwake bila kukamilika huku ujenzi ukiwa umeanza tangu 2012.

Elimu
Maoni