Waomba uhakiki mpya wa mipaka kati ya Tanzania na Kenya

|
Naibu waziri wa Mambo ya Nje ya nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na Naibu waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijazi wakikagua mpaka wa Jasini

Wakazi wa Kijiji cha Jasini Kata ya Mayomboni wilayani Mkinga, kilichopo mpakani mwa Kenya na Tanzania wameiomba Serikali kuhakiki upya mipaka iliyopo ili kuepuka muingiliano kwenye shuguli za kiuchumi ikiwemo suala zima la uvuvi.

Wameyasema hayo wakati wa ziara ya manaibu waziri wawili ambao ni Naibu waziri wa Mambo ya Nje ya nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na Naibu waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijazi waliofika kijijini hapo kwa lengo la kukagua mipaka hiyo.

Wakizungumza wakati wa ziara ya manaibu waziri hao baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wamesema wamekuwa katika mgogoro wa mara kwa mara na mamlaka za nchini Kenya katika muingiliano wa masuala ya uvuvi sanjari na kuiomba serikali iangalie uwezekano wa kuwajengea shule ili watoto wao waweze kusoma kijijini hapo badala ya kwenda upande wa Kenya ambao ndipo wanapopata elimu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Yona Mark amesema kwamba kwa upande wa elimu wanafunzi wanasoma Kenya lakini wamefanya jitihada za kujenga madarasa manne hivyo kwa sasa elimu ya msingi kuanzia darasa la kwanza mpaka la nne wanafunzi  wa kijiji hicho wanasoma Tanzania .

Kwa upande wake mara baada ya kufanya ziara na kuzungumza na watendaji wa kijiji hicho, Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kwamba Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Kenya itafanya zoezi hilo la uhakiki wa mipaka huku Naibu waziri wa Fedha na Mipango, Ashatu Kijaji akielezea namna ambavyo muingiliano huo unawapa changamoto kwenye ukusanyaji wa mapato na kuahidi kulifanyia.

Utawala
Maoni