Wasanii nchini waaswa kusikiliza nasaha za wakongwe

|
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo akizungumza katika hafla ya kumpongeza 'Monilisa'

Wasanii wa filamu nchini wameshauri kuheshimu na kuthamini mawazo na busara za wazee pindi wanapopata wasaa wa kukutana nao.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo wakati wa hafla ya kumpongeza Msanii wa Bongo Movie, Yvone Cherryl ‘‘Monalisa”  kufuatia kushnda tuzo muhimu za kutambua mchango wake zilizofanyika nchini Nigeria.

Fissoo alisema kuwa vijana wengi wa siku hizi hawathamini ushauri wa wazee na kufanya kama  desturi kutochukua ushauri au mawazo hayo kwa madai yamepitwa na wakati.

“Nikuombe mwanangu Monalisa nenda ukawe balozi mwema, waambie wenzako waenzi na kuheshimu busara za wazee, naamini kwa kufanya hivyo mtayaona mafanikio ya kazi zenu,”

Aidha Fissoo ameongeza kuwa Monalisa amekuwa msanii wa mfano wa kuigwa hasa katika nyanja ya maadili kitu ambacho wasanii wengi wanapaswa kuzingatia .

Naye  Yvone Cherryl ‘‘Monalisa” amesema kuwa anajisikia faraja kufika mbele ya watu ambao kwa namna moja ama nyingine walimtia moyo huku akiwa na ushindi ambao anaamini kuwa pamoja na juhudi zake binafsi maneno ya busara ya wazee hao yalimpa ari iliyosababisha kurejea akiwa mshindi.

“Nidhahiri kuwa maneno yenu ya busara ndiyo yametia chachu nikarejea nchini nikiwa mshindi wa Msanii Bora wa Kike Afrika, hivyo kwa kipekee sina budi kuwashukuru kwa duwa zenu na nitahakikisha naendelea kuenzi busara zenu,” alisema Monalisa.

Muigizaji  huyo wa Filamu nchini Tanzania, Yvonne Cherry maarufu kwa jina la Monalisa alishinda tuzo ya The African Prestigious Awards (APA) 2017 kwenye kipengele cha Msanii Bora wa Kike barani Afrika, Juma lililopita.

Filamu
Maoni