Watuhumiwa 12 waliotorosha dhahabu wapandishwa kortini

|
Watuhumiwa wa utoroshaji dhahabu mkoani Mwanza walipowasili Mahakamani Mwanza

Watuhumiwa 12 wakiwemo Polisi Wanane wanaotuhumiwa kuhusika na sakata la kusafirishwa kwa dhahabu iliyokamatwa Kilo 323.6 wamefikishwa Mahakamani na kusomewa jumla ya mashtaka 12 ikiwemo kuhujumu uchumi na kutakatisha fedha.

Miongoni mwa watuhumiwa hao  ni pamoja na polisi wanane wanaodaiwa kuhusika katika utoroshaji wa dhahabu zaidi ya  Kilogramu 300 pamoja na wafanyabiashara Sajid Hassan na Hassan Hassan wenye asili ya kiasia pamoja na Kisabo Kija Mkinda na Emanuel Ntemi.

Mbele ya Hakimu mkazi, Gwai Sumai , wanasheria watatu wa Serikali, Castus Ndamgoba, Robert Kidando na Jacline Nyantori, watuhumiwa hao wanasomewa mashtaka 12 yanayohusu uhumujumu uchumi, kuomba na kupokea rushwa sanjari na kutakatisha fedha katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Kagera na nchi jirani ya Rwanda.

Wakiwasomewa mashtaka hayo wanasheria hao wamewataja askari polisi wanane (8) wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Operesheni, Moris Okinda wakihusika kushiriki katika utoroshaji wa dhahabu licha ya kubaini kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Wamesema kuwa watuhumiwa hao pia wametenda kosa la kuomba na kupokea rushwa kiasi cha zaidi ya Millioni 700 kutoka kwa wafanyabiashara hao ambao walikuwa wakisafirisha dhahabu hizo bila kuwa na vibali sanjari kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.8.

Kati ya Januari 3- 5 watuhumiwa wote wanadaiwa kuhusika kutorosha dhahabu zaidi ya Kilogramu 300 bila vibali vya Serikali kabla ya kushukiwa na kukamatwa kwenye maeneo ya Kigongo feri na Kamanga wilayani Sengerema.

Kabla ya kufikishwa Mahakamani Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limewasimamisha kazi askari hao Wanane akiwepo aliyekuwa mkuu operesheni na wengine ni Daniel Kasara, Mtete Misana, Japheti Lukiko, Maingu Sorra, Alex Nkali, Timoth Nzumbi na David Ngelela wanaotuhumiwa kuhusika katika sakata hilo.

Mahakamani
Maoni