Watuhumiwa wa mauaji ya watoto Njombe wapandishwa mahakamani

|
Washtakiwa wa mauaji na kuteka watoto wa familia moja wakiwa mahakamani mkoani Njombe

Watuhumiwa wa mauaji ya watoto watatu wa familia moja yaliyofanyika Januari 20 katika Kijiji cha Ikando mkoani Njombe, wamefikishwa mahakamani leo, Jumanne kujibu tuhuma zinazowakabili.

Watuhumiwa hao walifikishwa katika viunga  vya Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Njombe majira ya mchana wakiwa katika ulinzi mkali wa askari polisi wakiwa imara huku kukiwa na makundi ya  wananchi waliojitokeza kushuhudia kesi za watuhumiwa hao wa  utekaji  na mauaji ya watoto yaliyotokea  mkoani Njombe.

Baadaye watuhumiwa hao walifika mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na kuingizwa katika chumba cha mahakama tayari kwa kusomewa mashtaka.

Ndani ya Mahakama, Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka na mawakili wa Serikali wakiongozwa na Wakili Mwandamizi Ahmed Seif pamoja naye Yahya Misango mbele ya Hakimu mkazi Magdalena Ntandu.

Watuhumiwa hao ni Joel Joseph Nziku mwenye umri wa miaka 35, Nasson Alfredo Kaduma  miaka 39 pamoja na Alphonce Edward Danda mwenye umri wa miaka 51 .

Akisoma maelezo ya awali ya kesi hiyo ya mauaji namba moja (1) ya mwaka 2019 inayowakabili watuhumiwa hao dhidi ya Jamuhuri, Wakili Ahmed Seif amesema watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa makosa matatu ya kuwaua watoto watatu ambao ni Godiliva Nziku aliyekuwa na umri wa miaka 11, kosa la pili ni la kumuua mtoto Gasper Nziku aliyekuwa na miaka minane (8) na la tatu ni la kumuua Giliad Nziku aliyekuwa na miaka mitano tukio walilolitekeleza Februari 20, 2019 katika Kijiji cha Ikando, Kata ya Kichiwa tarafa ya Makambako Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.

Mara baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa hawajaruhusiwa kujibu chochote mpaka shauri litakapofikishwa Mahakama Kuu kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi yao.

Watuhumiwa wamerudishwa rumande kwa kuwa kosa lao halina dhamana na wanatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Machi 25.

Kesi
Maoni