Wawindaji wa Dogon waua kabila la Fulani zaidi ya 100

|
Wananchi wa kabila la Fulani wakikimbia mapigano yanayoendelea kati ya Kabila la Dogon na Fulani nchini Mali

Wawindaji wa jamii ya Dogon wamewaua watu zaidi ya 100 katika shambulio lililofanyika katika kijiji cha watu wa kabila la Fulani katikati  mwa nchi ya Mali Jumamosi.

Idadi mpya imefikia watu 115 katika Kijiji cha Ogossagou.

Habari za kiusalama zimesema waathirika wa shambulio hilo walipigwa risasi au kukatwa kwa mapanga hadi kufa huku majeshi ya Mali yakisaidiwa na wakazi wa eneo waliwasili katika eneo hilo jana mchana.

Gavana wa eneo la Bankass, lililopo eneo la Ogossagou, Boubacar Kane, amesema idadi ya awali ni watu 115. Watu walionusurika wamewashutumu wawindaji hao wa kijadi kwa kufanya shambulio hilo.

Shambulio hilo lilifanyika mapema jana, Jumamosi karibu na mpaka na Burkina Faso. Eneo hilo limekuwa kitovu cha ghasia za kikabila nchini Mali.

Mauaji hayo yamefanyika wakati ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetembelea eneo la Sahel kutathmini hali ya tishio la wapiganaji wa Kiislam katika eneo hilo.

Wakati mashambulio hayo yakichochewa na Kabila la Fulani kuchunga mifugo yao katika ardhi ya Dogon na mgogoro wa kupata ardhi na maji, eneo hilo pia linakabiliwa na ghasia za wapiganaji wa Kiislam.

Katika miaka minne iliyopita, wapiganaji wa Jihadi waliibuka kuwa tishio katikati mwa Mali. Kundi hilo linaongozwa na mhubiri wa kiislam, Amadou Koufa ambaye amesajili wapiganaji wengi kutoka jamii ya Waislam wa kabila la Fulani.

Mauaji
Maoni